19 November 2012

Lukuvi: Kuvamiwa Mapadre Iringa kusihusishwe na migogoro ya kidini


Na Eliasa Ally, Iringa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Bw. William Lukuvi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Isimani, Wilaya ya Iringa Vijijini, amesema tukio la majambazi kuwavamia Mapadre wa Kanisa Katoliki jimboni humo na Paroko mmoja kupigwa risasi, halina uhusiano na migogoro ya kidini.

Alisema tukio hilo halina tofauti na ujambazi mwingine kama unaofanyika katika maeneo mbalimbali nchini katika hoteli,
benki, taasisi za serikali na binafsi.

Bw. Lukuvi aliyasema hayo mjini humo mwishoni mwa wiki
baada ya kumtembelea Paroko wa kanisa hilo, Parokia ya Lwang'a, Padre Angelo Burgio, aliyepigwa risasi katika ubavu wa kushoto na na Msaidizi wake Padre Helman Myala, alijeruhiwa kwa mapanga.

Mapadre hao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo ambapo
Bw. Lukuvi, alisema watu waishio vijijini hawajazoea kuvamiwa
na kupigwa risasi ambapo majambazi hao waliamini kuwa, kila anapoishi mzungu patakuwa na fedha.

Alisema matukio ya kuvamiwa kwa Misheni za Kanisa Katoliki mkoani humo yanatokea kwa nyakati tofauti ikiwemo Parokia za Idodi, Pawaga, Usokami na Isimani.

“Serikali itahakikisha matukio haya ya ujambazi ambayo yanaleta madhara makubwa kwa jamii yanakomeshwa hasa katika maeneo wanayoishi Wamisionari kwani ipo dhana iliyojengeka kuwa kila anapoishi mzungu huenda kuna fedha au mali ndivyo ilivyotokea kwa Mapadre wa Parokia ya Lwang'a,” alisema.

Alilitaka Jeshi la Polisi kutoa mafunzo kwa walinzi wanaolinda misheni zote wanazoishi Mapadre ili wawe na mbinu za kuwabaini kwa haraka majambazi na kuwathibiti kabla hawajaleta madhara.

Akizungumzia hali ya kiafya ya Mapadre hao, Mganga Msaidizi wa Hospitali ya Mkoa, Dkt. Faustine Gwanchele, alisema Padre Burgio ametolewa vipande vitano vya risasi mwilini baada ya kufanyiwa upasuaji na hali yake inaendelea vizuri pamoja na Padre Myala.

Alisema mlinzi aliyekuwa akilinda Kanisa la Kihesa Jimbo la
Iringa, Bathoromeo Nzigilwa, ambaye naye alicharangwa mapanga, amesafirishwa jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kutokana na hali yake ilikuwa mbaya.

No comments:

Post a Comment