27 November 2012

Kortini wakidaiwa kuisababishia serikali hasara



Na Rose Itono

MHANDISI Mkuu wa Mitambo na Meneja wa Fedha wa Shirika
la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu mashtaka mawili likiwemo la kuisababishia Serikali hasara
ya sh. milioni 120.


Mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi, Mwendesha Mashitaka wakili wa Serikali, Bw. Tumaini Kweka, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Wenceslaus Kamugisha (Mhandisi wa Mitambo), na Bi. Sarah Masiliso ambaye ni Meneja wa Fedha.

Bw. Kweka alidai mahakamani kuwa, Aprili 2011 tarehe isiyofahamika, katika maeneo ya TAZARA, washitakiwa wakiwa watumishi wa shirika hilo walitumia madaraka yao vibaya.

Shitaka la pili ilidaiwa washitakiwa wote kwa pamoja, Aprili 2011 katika tarehe isiyofahamika wakiwa watumishi wa shirika hilo, waliisababishia Serikali harasa ya sh. milioni 120.

Washitakiwa wote walikana mashtaka yao ambapo upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutotoa dhamana kwani kesi za aina hiyo zinahusu uhujumu uchumi na husikilizwa na Mahakama Kuu.

Hata hivyo, mawakili wa upande wa utetezi waliiomba Mahakama  kuwapa dhamana washtakiwa kwani sheria inaruhusu kufanya hivyo kama kesi hiyo haijafikishwa Mahakama Kuu.

Wakili wa mshtakiwa wa kwanza Bw. Mosha, alidai pamoja na
kesi hiyo kuwa ya uhujumu uchumi, bado sheria inaruhusu kwa kuzingatia vifungu vya dhamana.

Kabla Hakimu Moshi, hajakubali ombi la mawakili upande wa utetezi, alimpa nafasi wakili wa Serikali ambaye alidai kwa sababu dhamana ni haki ya mshtakiwa, wanaiomba Mahakama iweke masharti magumu pamoja na wadhamini wanaokubalika.

Hakimu Moshi aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili mmoja awe mtumishi wa Serikali au shirika linalofahamika ambao kila mmoja atasaini dhamana ya sh. milioni kumi.

Washtakiwa hao pia walitakiwa kuweka mahakamani dhamana ya sh. milioni 30 kila mmoja au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani hiyo na hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali.

Washitakiwa kwa pamoja walitoa hati ya thamani ya sh milioni 62 na wadhamini wawili kila mmoja ambapo wakili wa upande wa utetezi aliiomba Mahakama kuwapa muda wa kukagua barua na
hati za wadhamini ambapo kesi hiyo imepangwa kutajwa kesho.

No comments:

Post a Comment