21 November 2012

KESI YA MAUAJI DAR Wanajeshi 3 kunyongwa *Ni wale waliomuua mtoto wa Chifu Fundikira *Watiwa hatiani kwa ushahidi wa kimazingira


Na Rehema Mohamed

HUZUNI na vilio jana vilitawala katika Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam, baada ya mahakama hiyo kutoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa washtakiwa watatu waliotiwa hatiani
katika kesi ya mauaji ya Swetu Fundikira ambaye ni mtoto
wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira.

Washtakiwa hao ambao wote ni wanajeshi ni pamoja na MT 1900 Sajenti Roda Robert (42) wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni na wenzake, MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37)
wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid (JKT Mbweni).

Vilio hivyo vilitawala mahakamani hapo baada ya Jaji Zainab
Mruke aliyekuwa akiisikiliza kusoma hukumu ambayo iliwatia hatiani washtakiwa wote kwa ushahidi wa kimazingira.

Jaji Mruke alisema, upande wa mashtkata umeweza kuthibitisha
kesi yao bila shaka na hivyo mahakama imeona kuwa, washtakiwa wote wanahatia na walimuua marehemu Fundikila kwa kukusudia.

Alisema katika mazingira ya kesi hiyo, ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka umeungana pasipo kuacha shaka licha ya kuwa na ushahidi wa kimazingira.

“Pamoja na kwamba ni ushahidi wa kimazingira, umejitoshereza kwa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi yao na kuweka mnyororo usiokuwa na matundu,” alisema Jaji Mruke.

Aliongeza kuwa, katika ushahidi huo washtakiwa hao walionekana kuwa na nia ovu na kumuua marehemu Fundikira baada ya Sajenti Robert kumwambia marehemu na mwenzake kuwa “msipowa heshimu wakubwa wa nchi hii mtapata shida”.

Alitaja viashiria vingine vya nia ovu kuwa ni pamoja na pale marehemu alipokutwa mtupu bila nguo akiwa amelala kifudifudi pembeni mwa barabara na hajitambuni akipumua kwa shida huku washtakiwa wakiwa pembeni yake.

Alisema kilichompata marehemu kilitakiwa kielezwe kwa kina
na washtakiwa hao ambapo katika ushahidi wao hawakutoa
maelezo hayo na yale waliyotoa hayaaminiki na kutia shaka.

Jaji Mruke alisema shahidi wa nne upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambaye alikuwa Daktari aliyeuchunguza mwili wa marehemu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alieleza kuwa marehemu Fundikira alikufa kutokana na majeraha ya kichwa.

Alisema katika ushahidi wake, shahidi huyo aliieleza Mahakama hiyo kuwa majeraha hayo yalitokana na mgandamizo wa kitu cha ubapa katika kichwa chake, kusababisha damu kuvilia kichwani
na damu nyingine kuganda upande mmoja wa kichwa.

Baaada ya kusomwa hukumu hiyo, ndugu wa marehemu waliangua kilio cha uchungu wakidai kutoneshwa kidonda cha kufiwa na ndugu yao ambaye aliuawa kinyama.

Wakili wa utetezi Bw. Mruge Karoli, alisema hawajaridhika na hukumu hiyo hivyo watakata rufaa.

Kesi ya msingi:

Januari 23 ,2010 katika eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa hao walidaiwa kumuua marehemu Fundikila

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita  ambapo katika usikilizwaji wa awali, washtakiwa wote walikana kutenda kosa hilo.

Upande wa mashtaka uliwajibika kuleta mashahidi wa kuthibitisha kesi hiyo ambapo mambo yaliyotakiwa kuthibitishwa ni pamoja na kama kifo hicho hakikuwa cha kawaida na kuthibitisha washtakiwa hao kuhusika na mauaji hayo wakiwa na nia ya ovu.

Katika kuthibitisha nia ya ovu, Jaji Mruke alisema lazima izingatiwe kama kulikuwa na siraha yoyote iliyotumika au nguvu katika matumizi ya silaha husika.

Uthibitisho mwingine uliohitajika mahakamani ni aina ya siraha iliyotumika, idadi ya majeraha, mapigo ya majeraha na tabia za washtakiwa kabla na baada ya tukio.

Ushahidi upande wa mashtaka:

Katika kesi hiyo, inadaiwa Januari 23,2010, majira ya saa sita usiku, marehemu akiwa na wenzake wawili kwenye gari aina ya Toyota Corolla, wakitokea Mwananyamala, walikutana na washtakiwa
hao eneo la Kinondoni wakiwa katika gari lao wakitokea kwenye maegesho ya magari Baa ya Mango Garden.

Ilidaiwa kuwa, mshtakiwa wa kwanza (MT 1900 Sajenti Robert), alimwamuru dereva wa gari alilokuwa marehemu, arudi nyuma
na dereva huyo kutii amri hiyo.

Washtakiwa hao walilifuata gari hilo ambapo mshtakiwa wa kwanza (MT 1900 Sajenti Robert), alishuka katika gari lao kumfuata dereva wa gari aliyopanda marehemu na kumuonya kuwa “siku nyingine asipo waheshimu viongozi wa nchi atapata shida”.

Baada ya kutoa maneno hayo, marehemu na wenzake waliondoka lakini walipofika kwenye makutano ya Barabara ya Kawawa na Mwinyijuma, walikutana tena na washtakiwa ndipo MT 1900
Sajenti Robert, akawatukana na kuwaambia “wale washenzi
hawa hapa, niliwaambia tuwashughulikie mkakataa,
si mnaona wametufuata?”

Inaelezwa kuwa, marehemu aliuliza sababu ya kuwatukana bila kosa, lakini badala yake mshtakiwa Koplo Ngumbe na Koplo Rashid walitelemka ndani ya gari na kuanza kumpiga dereva wa gari lao hivyo marehemu alilazimika kwenda kumsaidia asipigwe.

Kitendo hicho kilisababisha ugomvi huo kuamia kwa marehemu ndipo alipochukuliwa na washtakiwa kwa madai ya kumpeleka
Kituo cha Polisi Ostarbey.

Kabla washtakiwa hao hawajaondoka na marehemu katika eneo la tukio, alifika Bw. Beni Kinyaiya, ambaye alikuwa shahidi wa pili katika kesi hiyo na kuhoji kinachoendelea.

Sajenti Robert alimjibu Bw. Kinyaiya kuwa mambo hayo hayamuhusu na kama anataka kujua aende Kituo cha Polisi
Ostabey na alipokwenda kituoni hapo kuulizia tukio hilo,
akaambiwa halipo hivyo aliamua kuondoka.

Askali polisi wa Kituo cha Salenda, walipata taarifa kutoka kwa dereva wa taksi aliyepita kituoni hapo aliyewaeleza kuwa kulikuwa na watu wakipigana katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Kutokana na taarifa hizo, askari hao akiwemo mwenye namba
T 1747 Deoscas, walifika eneo la tukio na kumkuta marehemu pembezoni mwa barabara hiyo katika Msikiti wa Jamat akiwa amelala chini kifudifudi, hapumui vizuri, soksi moja mguu wa
kulia na hakuwa na nguo (mtupu).

Katika ushahidi wake, Deoscas alisema pembeni ya marehemu alisimama Sajent Robert ambaye alikuwa akizungumza kwa
hasira na kusema “huyu ni mshenzi sana, ametusumbua
kwa muda mrefu”.

Mshtakiwa wa pili, Koplo Rashidi alishuka kwenye gari lao ambalo lilikuwa eneo la tukio hatua sita kutoka alipolala marehemu na kutoa maelezo kuwa, walikuwa wanampeleka marehemu Kituo cha Polisi Kati (Central), baada ya kutaka kuwaibia gari lao na baadaye akaruka kutoka ndani ya gari hilo.

Deoscas alipohoji uwepo wa marehemu bila nguo, Sajenti Robert alidai zimo ndani ya gari na polisi walipotaka kufahamu nani alimvua nguo hizo walidai alivua mwenyewe wakati akitaka kuruka ndani ya gari lao ili akimbie.

Afande Deoscas alidai baada ya hapo, aliwachukua washtakiwa
hao hadi Kituo cha Polisi cha Salenda ambako alikutana na Bw. Kinyaiya na wenzake ambao waliwaeleza polisi kuwa
wanamjua marehemu ambaye ni jamaa yao.

Katika maelezo ya mpelelelzi wa kesi hiyo ambaye alikuwa shahidi wa sita, aliieleza Mahakama hiyo kuwa washtakiwa wote walikiri kupigana na marehemu na walikutana naye Msikiti wa Jamat.

Alisema katika maelezo yao, washtakiwa hao walikana kuhusika
na kifo chake na kudai aliruka mwenyewe kutoka ndani ya gari
ili asipelekwe Kituo cha Polisi.

Utetezi wa washtakiwa:

Katika utetezi wao washtakiwa hao walidai walikuwa wanampeleka marehemu Kituo cha Polisi Kati kwa sababu ndiyo kituo pekee walichokuwa wakikijua licha ya kuishi Dar es Salaam kwa miaka zaidi ya 20.

Washtakiwa hao pia walikiri kukutwa na marehemu akiwa hajitambui, bila nguo na mguu wa kulia akiwa na soksi.

Sheria:

Jaji Mruke alisema, sheria ipo wazi kuwa kama utaondoka na mtu akiwa hai na wewe ni mtu wa mwisho kuonwa naye, baadaye mtu huyo akipatwa na matatizo, mtu wa mwisho kuonwa naye atawajibika kueleza kilichompata.

Alisema kwa maana hiyo, Mahakama ilijiuliza kama maelezo yaliyotolewa na washtakiwa yalijitoshereza.

“Muda wa saa 8 usiku Msikiti wa Jamat si watu wengi wanaopita eneo hilo, muda huo eneo hilo huwa tulivu sana hicho ni kiashiria cha washtakiwa kujieleza kwa kina,” alisema.

“Washtakiwa walipita vituo viwili vya polisi kutoka makutano ya Barabara ya Kawawa na Mwinyijuma ambavyo ni Ostarbay na Salenda, kwanini hawakumpeleka katika vitu hivyo kama walivyosema awali?,” alihoji Jaji Mruke.

Aliongeza kuwa, ushahidi wa washtakiwa kuwa walikuwa wanampeleka marehemu Kituo cha Polisi Kati unatia shaka
na ndio unaofanya wajieleze kwa kina.

Jaji Mruke alisema maelezo ya kina ya washtakiwa yanasema, marehemu alianguka kwa kuruka ndani ya gari ambapo Afande Deoscas alisema kama marehemu angeruka na kuanguka, angeangukia mbali na barabara pia agekuwa na mpasuko.

“Haiwezekani askari watatu washindwe kumdhibiti marehemu hadi avue nguo na kuruka kutoka ndani ya gari huku wakimuangalia na kwamba utetezi wao ni utata,” alisema Jaji Mruke na kuongeza kuwa maelezo ya washtakiwa hayaaminiki na yanatia shaka licha ya kutokuwepo shahidi aliyeshuhudia marehemu akiuwawa.

4 comments:

  1. hao jamaa ni haki yao kunyongwa!!! baadhi ya askari wa jeshi hua wanatumia madaraka yao vibaya na kuonea wananchi na mimi nafikiri kama wao ndio wahusika wa tukio hilo basi nao walitumia madaraka yao vibaya!!!wanastahili adhabu hiyo!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Wanyongwe tu. Ushahidi umetosha kabisa, na wameshindwa kujitetea maelezo yao ni ya kitoto. Miaka ishirini Dar hawavijui vituo vya Jeshi la Polishi na wao ni wanajeshi. Wanyongwe mpaka wafe tena haraka saaaaaana.
    Jirani wa Marehemu Swetu.

    ReplyDelete
  3. Hawa jamaa wamezidi wanajifanya wao ni kila kitu,Sheria ichukue Mkondo wake, wamezoea uonevu, hawana utu...

    ReplyDelete
  4. Hadi kuuwa wanyongwe na hadharani ni uonevu mkubwa haukubaliki hata kidogo

    ReplyDelete