21 November 2012

Elimu bure sera ya CCM - Nape *Wadau wampinga Lowassa, wadai inapotosha



Na Waandishi Wetu

SIKU moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, kuitaka Serikali ione umuhimu wa kutoa elimu ya sekondari bure, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa ufafanuzi wa kauli hiyo.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, alisema sera ya kutoa elimu bure kwa shule za sekondari ni miongoni mwa maazimio yaliyojadiliwa katika Mkutano Mkuu wa Nane wa chama hicho uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

Bw. Nape aliyasema hayo Dar es Salaam jana akizungumzia ziara
za Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurahman Kinana, katika mikoa minne kuanzia Novemba 21 mwaka huu.

“Kama kuna mtu ameyasema haya sio mawazo yake bali ya chama, ambayo yalifikiwa katika Mkutano Mkuu wa CCM ili kupunguza mzigo wa upatikanaji elimu ya sekondari,” alisema.

Akizungumzia ziara hiyo, alisema Bw. Kinana ataongozana na wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho pamoja na baadhi ya Mawaziri na itaanzia mkoani Mtwara.

Alisema timu hiyo itakwenda kuangalia maendeleo ya zao la korosho, madini na mambo mengine ya maendeleo na baada ya
hapo, Novemba 22 watakwenda Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Aliongeza kuwa, wakiwa mkoani humo wataangalia miundombinu hasa ya barabara pamoja na kuzungumza na wana CCM ambapo Novemba 23 watakwenda Geita, ambako watangalia shughuli za uchimbaji wa madini na changamoto walizonazo wachimbaji
wadogo wadogo.

“Novemba Novemba 24 mwaka huu, watakuwa jijini Arusha ambapo lengo la safari zote ni kuangalia hali ya maendeleo kila Mkoa na kufanya tathmini juu ya utekelezaji wa ilani ya chama,” alisema Bw. Nnauye.

Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo Mawaziri watatakiwa kutoa maelezo katika maeneo ambayo wananchi watahitaji ufafanuzi
wa mambo mbalimbali pamoja na kuzungumza na wana CCM.

Akiizungumzia CHADEMA ambayo imeponda uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Bw. Philip Mangula, alisema yeye angeshangaa kama chama hicho kingetoa pongezi zozote.

“Kama Dkt. Slaa ataponda uamuzi wetu kwetu ni furaa maana wanajua kisiki tulichokiweka si cha mchezo,” alisema.

Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali wa elimu nchini, nao wameikosoa kauli ya Bw. Lowassa ya kuitaka Serikali itoe elimu bure kwa shule za sekondari.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti Dar es salaam jana, baadhi ya wadau hao walisema kauli hiyo inapotosha jamii ambayo inafahamu kwa kiasi gani kuna umuhimu wa kuchangia gharama za elimu ili kuwezesha wanafunzi kupata elimu bora.

Ofisa kutoka Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) ambaye hakutaka
jina lake liandikwe gazetini, alisema Watanzania wanahitaji elimu bora hivyo lazima kuwepo na gharama kidogo.

Aliwataka wananchi kuondokana na fikra potofu za kisiasa kuwa elimu ya sekondari inaweza kutolewa bure na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo ni kuibebesha Serikali mzigo mkubwa.

“Kama Watanzania tunahitaji elimu bora lazima tuchangie gharama zake kwani bila kuchangia ni kuibebesha Serikali mzigo,  katika shule za msingi Serikali imiweza kuitoa bure kwa sababu ya miundombinu yake na gharama za uendeshaji.

“Lowasa asitake kupotosha jamii, kama tunahitaji elimu bora lazima tuichangie lakini kama tunataka bora elimu wanayoizungumia baadhi ya wanasiasa kwenye majukwaa ikiwemo watoto kusoma katika mazingira magumu inawezekana kutolewa bure,” alisema.

Aliongeza kuwa, wananchi wanapaswa kuelewa kuwa, hivi sasa
nchi imefikia hitaji la wanafunzi milioni moja kwa mwaka ambao wanahitajika kujiunga na elimu ya sekondari wakati miundombinu, posho na mishahara ya walimu ikiwa ni sehemu ya changamoto.

Mdau huyo alisema, sambamba na changamoto za mishahara ya walimu, vifaa vya kufundishia navyo ni tatizo kwa upande wa uwezeshwaji wa elimu ya vitendo hivyo Serikali ikiondoa
uchangiaji elimu ya sekondari robo tatu ya bajeti lazima
ielekezwe katika elimu.

“Tukieleleza robo tatu ya bajeti ya Serikali katika elimu sasa maeneo mengine itakuwaje, upo umuhimu wa jamii kuchangia katika sekta ya elimu ili kuipunguzia mzigo Serikali,” alisema mdau huyo.

Naye Mlezi wa Chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC) Kanda ya Kaskazini, Hassa Doyo alisema hakubaliani na pendekezo la Bw. Lowassa na kudai huo ni upotoshaji mkubwa.

Alihoji kama Bw. Lowassa aliona ni rahisi Serikali kutoa elimu
bure kwa shule za sekondari kwa nini hakufanya hivyo
wakati akiwa Waziri Mkuu.

“Kipindi kile akiwa Waziri Mkuu, ilikuwa rahisi kuishawishi Serikali aliyokuwa akiiongoza na kuonesha uhodari wake katika utekelezaji lakini hiki anachokisema sasa ni ndoto,” alisema.

Alisema ni wajibu wa wana CCM kutafakari kwa kina kauli ya
Bw. Lowassa kwani ameonesha kupingana na sera za chama
chake na kuunga mkono za wapinzani.

“Sera hii inatumiwa na chama kimoja cha siasa nchini (akimaanisha CHADEMA), katika kusaka uongozi bila kujua athari za sera hiyo kwani itachangia kushuka kwa kiwango cha elimu,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila, alisema suala la wanafunzi wa sekondari kusoma bure haliwezekani kutokana na rasilimali nyingi kuwa mikononi mwa mikono ya watu wachache kwa maslahi yao.

Alitolea mfano wa rasilimali zilizopo mikononi mwa watu wachache kuwa ni madini ya aina mbalimbali yenye thamani kubwa ambayo hayapatikane nchi nyingine duniani pamoja na nishati.

“Kama rasilimali hizi zingetumika kunufaisha Watanzania wote, uchumi wa nchi yetu ungekua na umaskini ungekwisha,” alisema.

Imeandikwa na Darlin Said, Mariamu Mziwanda, Rose Itono na Rehema Maigala.

No comments:

Post a Comment