26 November 2012

Bilal kuweka jiwe la msingi nyumba za gharama nafuu NHC


Na Rachel Balama

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi kwenye mradi wa nyumba 94 za makazi za Shirika la Nyumba la  Taifa (NHC) zilizopo katika eneo la Ilembo mjini Mpanda, mkoani Katavi.


Akizungumza kwa njia ya simu akiwa mjini Mpanda Meneja Mawasiliano wa NHC, Bw.Yahya Charahani alisema Makamu wa Rais ataweka jiwe hilo la msingi katika mradi huo Mradi ulioanza Novemba 2012, na unategemewa kukamilika Februari 2013 ikiwa ni muda wa takribani mwaka.

Alisema mradi huo una nyumba za gharama nafuu 94 tu zitakazouzwa, kuna nyumba za vyumba vitatu vya kulala na zingine zina vyumba viwili vya
kulala, sebule, jiko la kisasa na maegesho ya magari ya ziada. Nyingi kati ya hizo zitakuwa ni zile za vyumba vitatu.

Alisema mradi una nyumba 94 zitakazogharimu kiasi cha Sh. bilioni 3.8 ikiwa ni wastani wa Sh.milioni 40 kila jengo.

Alisema fedha za ujenzi wa mradi huo zimetokana na mkopo kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Makazi la
Shelter Afrique wa kiasi cha Sh.bilioni 24.

Alisema mkandarasi Msimamizi wa mradi huo ni Shirika lenyewe, ambapo kazi zote za usanifu , uhandisi na ukadiriaji wa gharama za ujenzi
zimefanywa na wataalamu wa vitengo mbalimbali vya Shirika la Nyumba la Taifa.

Naye Meneja wa NHC Katavi, Bw.Nehemia  Msigwa,alisema kuwa ujenzi huo umeanza kwa kujenga nyumba 20 hadi sasa kwa maana ya kuchimba misingi
na kuanza kuinua ukuta.

Alisema kuwa nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala na zingine zina vyumba viwili sebule, jiko na choo cha umma zinatarajiwa kukamilika Mei, mwakani.

Alisema zitakapokamilika nyumba hizo zitauzwa kwa wananchi wa mkoani Katavi ili kupunguza matatizo ya makazi kwa wananchi wa mjini Mpanda.

Akizungumza wakati akikagua mabanda ya maonyesho ya taasisi na asasi mbalimbali za umma na zisizokuwa za kiserikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilipongeza Shirika la Nyumba kwa uamuzi wa kuupa kipaumbele Mkoa mpya wa Katavi, kwa kuwajengea nyumba za gharama nafuu.


No comments:

Post a Comment