08 October 2012
Waya mpya wa umeme utakaolazwa baharini wawasili Zanzibar
Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar
HATIMAE waya mpya wa umeme utakaolazwa baharini kutoka Ras Fumba Zanzibar hadi Ras Kiromoni Dar-es-Salaam umewasili Zanzibar na kupokewa rasmi pamoja na kukaguliwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, katika bandari ya Malindi mjini Unguja.
Waya huo utakaotumika katika mradi wa uwekaji wa waya wa pili wa umeme kutoka Ras-Fumba hadi Ras Kiromoni Dar-es-Salaam, shughuli zake za ulazaji zinatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu asubuhi.
Akitoa maelezo yake huku akionesha furaha kubwa Dkt. Shein alitoa pongezi kwa Kampuni na Wakandarasi waliotengeza waya huo alieleza kuwa
licha ya kazi hiyo kuwa ngumu lakini imefanywa vizuri.
Dkt. Shein alisema kuja kwa waya huo kutapunguza usumbufu wanaoupata hivi sasa wananchi wa kupata umeme kwa mgao kwani waya huo utakuwa na umeme wenye megawati 100 ambazo zitatosheleza kwa kiasi kikubwa na nyingine kubakia.
Alisema matumizi ya umeme kwa kisiwa cha Unguja ni megawati 45 tu kwa hivi sasa,lakini waya una megawati 100 ambazo zitasaidia kutoa huduma hiyo pamoja na kuweza kujipanga vizuri kwa shughuli nyingine za maendeleo hapo baadae.
Dkt. Shein alisema kuwa waya huo ambao pia, utasaidia kutoa huduma nyingine za mawasiliano yakiwemo mtandao wa intaneti utawezesha kutoa huduma za e- Government pamoja na huduma za mkonga wa Taifa kama ulivyo kwa waya uliolazwa kisiwani Pemba.
Dkt. Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ulazaji wa waya huo katika hafla itakayofanyika siku ya Jumatatu asubuhi.
Akipata maelezo kutoka kwa jopo la wakandarasi wa waya huo Kampuni ya VISCAS, na mhandisi mdogo pamoja na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya ESB International pamoja na Msaidizi Mtendaji Mkuu wa MCA-T kwa upande wa Zanzibar Bw. Ahmed Rashid,
walieleza kuwa shughuli hizo za ulazaji wa waya zitafanywa si zaidi ya siku 12 kwa kutumia meli na vifaa walivyonavyo kwa kushirikiana na meli nyengine.
Walieleza kuwa waya huo wenye urefu wa kilomita 37 na uzito wa tani 2000, shughuli za ulazaji pamoja na zile za kuunganisha katika vituo maalum vilivyopo Mtoni na vile vya Dar-es-Salaam zinatarajiwa kumalizika na kutoa huduma ya umeme unatokana na waya huo mpya mnamo mwanzoni mwa mwezi wa Novemba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment