08 October 2012
Kampuni uchimbaji madini kufutiwa leseni
Na Agnes Mwaijega
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini Bw.Stephen Masele, amesema Serikali haitakuwa tayari kuendelea kuzivumilia kampuni zinazohusika na uchimbaji wa madini ambazo hazilipi kodi naamesisitiza kuwa zitafutiwa leseni.
Pia amesema Wizara ya Nishati na Madini imeshaunda timu ya wataalam kwa ajili ya kupitia upya mikataba ya kampuni mbalimbali zinazohusika na uchimbaji wa madini nchini.
Bw.Masele aliyasema Dar es Salaam juzi alipokuwa akizindua taarifa ya haki za binadamu na uwekezaji nchini iliyotolewa na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
Alisema wamebaini mambo mengi baada ya kutembelea migodi mbalimbali na kuonya kuwa kama hatua hazitachukuliwa mapema taifa litaendelea kupoteza fedha nyingi huku Watanzania wakizidi kuteseka kwa umasikini.
Wakati huo huo, alisema wizara tayari imeshasitisha utoaji wa leseni mpya kwa kampuni za uchimbaji wa gesi ili ziweze kupitiwa kwanza.
"Miongoni mwa mambo mazuri katika taarifa hii ni kuhusu suala zima la wajibu wa kulipa kodi na ikumbukwe kwamba mara zote tunapojadili haki za binadamu ni vyema pia kuzungumzia wajibu wa binadamu kwa wenzake na kwa Serikali.
"Tumechoka kuona kwamba taifa letu linageuzwa na kuwa shamba la bibi ndiyo maana tumeamua kufanya mapinduzi makubwa, hata waziri amesema wazi mikataba yote inayohusisha wizara sasa hivi itasainiwa hapa hapa tena kwa uwazi," alisema.
Akizungumzia kuhusu mazingira ya wafanyakazi wa migodini ambayo ni magumu alisema wizara imejipanga kutembelea migodi yote na kuhakikisha kampuni hizo zinazingatia maslaia yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment