02 October 2012
Uchaguzi CCM usiwe kufa na kopona-Pinda
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wanagombea nafasi mbalimbali za uongozindani ya chama hicho, wasiligeuze suala la uchaguzi kuwa ni la kufa na kupona.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana katika vyombo vya habari, ilisema Bw. Pinda aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Katavi, katika mkutano uliofanyika Shule ya Sekondari ya Milala, iliyopo wilayani Mpanda.
Alisema viongozi waliochaguliwa na waliokosa uongozi waache kinyongo baada ya uchaguzi.
“Tunapoomba nafasi hizi tusiligeuze suala hili kuwa ni la kufa na kupona, huko tunakotaka kwenda kuna nini? Kwanini tunawekeana kinyongo baada ya uchaguzi wakati hii ni nafasi tu ya kuwahudumia
wana CCM,” alihoji Bw. Pinda.
Bw. Pinda ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM, aliwataka wagombea wa nafasi mbalimbali wawe tayari kupokea matokeo kwa moyo mkunjufu na kuvunja makundi baada ya uchaguzi huo kukamilika.
Katika taarifa hiyo, Bw. Pinda alisema Wilaya za Mpanda ziligawanywa kwa mara ya kwanza baada ya kuundwa Mkoa mpya wa Katavi.
Aliwataka viongozi ambao watashinda uchaguzi huo wafuatilie kwa makini utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kudai taarifa za maendeleo kutoka kwa watendaji wa vijiji na kata kila baada ya miezi mitatu.
“Katibu wa Tawi una wajibu wa kumwandikia barua Mtendaji wa Kijiji (VEO) na kudai taarifa za miezi mitatu ambazo zitaonesha mapato na matumizi...asipofanya hivyo, unamwandikia barua ya kumkumbusha na asipotekeleza, peleka taarifa ngazi ya juu.
“Nasi tukipewa taarifa tutuazishughulikia, tukitimua wawili watatu, heshima ya kazi itarudi,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment