02 October 2012
Siku ya wazee iadhimishwe kwa kusherehekea mafanikio si matatizo
Na Rabia Bakari
KILA ifikapo Oktoba mosi ya kila mwaka, wazee wa Tanzania wanaungana na wazee wengine duniani kuadhimisha siku yao.
Katika maadhimisho hayo, wazee hutoa vilio vyao vya matatizo yanayowakabili kwa mamlaka husika ili yaweze kufanyiwa kazi na kumalizwa kabisa, kwa sababu viongozi muhimu na wadau wa wazee huwepo siku hiyo.
Kutokana na mafanikio hafifu ya kumalizwa kero zinazowakabili wazee, imekuwa ni kawaida sasa, kwenye
maadhimisho hayo kupambwa na malalamiko ya kero tu, ikiwemo kutothaminiwa katika jamii, vitendo vya ukatili na ukosefu wa huduma za afya.
Hiyo haimaniishi kuwa serikali haifanyi chochote, la hasha. Imesimamia matatizo ya wazee kwa kadri ilivyoweza, ikiwemo kuhakikisha huduma za afya zinapatikana bure kwa wazee wote na kutungwa kwa sera ya kuwalinda.
Na wadau nao kwa upande wao yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, yamepambana kwa kila hali kuhakikisha haki za wazee zinalindwa na kufanyiwa kazi na jamii.
Juhudi zipo, yapo yaliyofanyika, lakini nguvu kubwa inahitajika ili angalau kumaliza nusu ya matatizo yanayowakabili.
Ofisa kutoka shirika lisilo la kiserikali linalosimamia
mambo ya wazee la Help Age international, Bw.Leonard Ndamguba anasema kuwa, wamejitahidi kusimamia kuhakikisha wazee wote wanapata pensheni bila kujali alikuwa ni mfanyakazi katika sekta rasmi au la, ili angalau pensheni hiyo impe unafuu wa maisha wa kumudu mambo ya msingi, kwa kuwa wazee nao walishiriki ujenzi wa taifa kwa namna moja ama nyingine.
Sambamba na hilo, anasema kuwa wameungana na wadau kuhakikisha kuwa sera ya wazee ya mwaka 2003 inapitishwa
na kuwa sheria, ili mambo mengi yanayohusu wazee
yasimamiwe kisheria.
"Tunataka mwaka huu tusisheherekee tena matatizo bali
mafanikio na namna changamoto zinazowakabili wazee
zilivyofanyiwa kazi.
"Yapo mambo mengi yanayotakiwa kusimamiwa kikamilifu na
hatimaye kuwa yenye mafanikio makubwa ikiwemo la wazee kupata pensheni kwa mujibu wa sheria baada ya sheria ya wazee kupitishwa, lakini kubwa linalotakiwa kusimamiwa na kumalizwa kabisa ni haki ya kuishi ambayo wazee wengi wamenyimwa kutokana na mauaji ya kikatili wanayofanyiwa, "anasisitiza.
Akifafanua kuhusu hilo, anasema wazee wengi wamekuwa
wakiuawa kikatili kwa imani za kishirikina, na wakati
huo hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa, hali
inayozidi kutia shaka kila siku juu ya wazee wengi waliopo vijijini.
Naye Bi. Theresa Minja akitoa msimamo kwa niaba ya wazee
wengine anasema kuwa maelfu ya wazee wamepoteza maisha
katika sehemu mbalimbali za nchi hii kwa kutuhumiwa kuwa wachawi.
"Jambo la kusikitisha ni kuwa mauaji hayo yamekuwa yakifanyika kikatili mno kwa kutumia mapanga, mawe,
mashoka na silaha nyingine. Baadhi ya wazee hasa usukumani wamefukuzwa kwenye nyumba zao, wametengwa kwa kutuhumiwa kuwa ni wachawi na hivyo kulazimika kukimbilia na kuishi kama ombaomba kwa kuhofia kuwa na wao wangevamiwa na kuuawa,"anasema.
Hali ya unyama na ukatili uliokithiri inatisha na kuamsha hamasa kwa watanzania hasa wakati nchi ikiwa kwenye sifa kubwa ya misingi ya utawala. Hali hiyo inaharibu jina la nchi
ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na kuwavunja moyo wazee ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kupigania maendeleo ya nchi.
Bi. Minja anasema kuwa inasemekana kuwa kabla ya uhuru
imani za kichawi zilikuwepo katika jamii nyingi za Afrika, lakini vitisho vya uchawi vilikuwa vikishughulikiwa kulingana na tamaduni na mahali husika bila kuwaua
watuhumiwa.
Hata hivyo kati ya mwaka 1970 na 1988 jumla ya watu 3, 073 waliuawa katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza baada ya
kutuhumiwa kuwa ni wachawi na kuanzia hapo mauaji hayo yamekuwa yakiripotiwa na kuongezeka kila kukicha ikiwa ni pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa imani ile ile mnamo miaka miwili iliyopita.
Katika ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
ya mwaka 2011 imeonesha kusambaa kwa mauaji katika mikoa mingine sita na imeonesha kuongezeka kwa mauaji kutoka 579 mwaka 2010 hadi 642 mwaka 2011.
Tafiti mbalimbali zimefanywa na serikali pamoja na wadau wengine ikiwa ni pamoja na asasi za haki za binadamu, Help Age International, TAMWA, Tume ya Nyalali na Dkt.
Mesaki wa Chuo Kikuu Dar es Salaam lengo likiwa ni kuelewa chanzo na hali ya mauaji ya wazee kwa tuhuma za ushirikina nchini.
Anasema kuwa matokeo ya tafiti hizo yaligundua sababu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya jinsia, matatizo ya kiafya, wivu, umaskini, hali mbaya ya hewa, ugomvi wa mali na urithi, uelewa mdogo kuhusu Virusi Vya UKIMWI na
UKIMWI.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawahakikishia ulinzi na haki ya kuishi raia wake, pia serikali imeridhia mikataba ya Umoja wa Mataifa (UN) inayolinda haki za wanawake, pia sera ya taifa ya wazee pamoja na MKUKUTA
inaelekeza jinsi masuala ya wazee yatakavyoshughulikiwa japo bado haijashughulikia suala la mauaji ya wazee.
"Kimsingi sera ya taifa ya wazee ndiyo sera pekee inayolaumu mila potofu ikiwa ni pamoja na mauaji ya wazee kwa tuhuma za uchawi, hata hivyo sera hiyo bado haijatungiwa sheria tangu
mwaka 2003 hivyo kukosa nguvu za kisheria kukabiliana na mauaji ya wazee.
"Tanzania inazo sheria zake ambazo hushugulikiwa na mahakama. Hii ni haki kwa wananchi wote, lakini inaonekana sio hivyo kwa wazee wanaotuhumiwa uchawi. Mbaya zaidi kesi nyingi zinazohusiana na mauaji ya wazee zimekuwa zikiishia njiani kwa maelezo ya kukosa ushahidi wa kutosha. Hii imechangia kuendelea kuuawa,"anaongeza.
Jitihada, mikakati, mbinu na kampeni mbalimbali zimefanyika na wadau ikiwa ni pamoja na serikali, watu binafsi, mashirika ya dini, asasi na mashirika ya kimataifa ili
kukabiliana na tatizo hilo, lakini pamoja na juhudi hizo mafanikio bado hayajaonekana.
Jamii imeweza kutumia njia zao ikiwa ni pamoja na kutumia sungusungu na waganga wa jadi kusaidia juhudi hizo, lakini hali bado tete.
Vitendo vya mauaji ya wazee vinazidi kuongezeka na kusambaa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, takwimu kutoka kwa wadau
mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali zinaonesha kuwa kati ya mwaka 1998 hadi 2001 kulikuwepo na matukio 17,220 ya kuwadhalilisha wazee na mauaji 1,746 kutokana na imani za
kishirikina.
Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2009 ilionesha kuwa wanawake wazee 2,583 walikuwa wameuawa katika mikoa minne nchini ikiwa ni wastani wa mauaji 517 mwaka.
Ripoti hiyo ilionesha kuwa mwaka 2010 idadi ya mauaji 2,866 kuanzia mwaka 2003 hadi 2008, takwimu za mkoa wa Mwanza pekee ambao ndio ulikuwa na mauaji mengi nchini zilionesha kuwa wanawake wazee 689 waliuawa kati ya mwaka 2002 hadi 2007 ikiwa ni wastani wa mauaji 140 kila mwaka.
Anasisitiza kuwa jamii itambue kwamba taarifa za kutisha
kwa mauaji ya wazee zinaondoa imani na amani katika mioyo ya wazee, na mfano mwingine ni kutoka Shinyanga ambapo zinasema wanawake wazee 242 waliuawa mkoani humo kati
ya Januari 2010 na Juni 2011.
Wakati mauaji yaliyo mengi yanatokea mikoa ya Mwanza na
Shinyanga, na takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa tatizo la mauaji linasambaa mikoa mingine.
Haki za wazee zimeendelea kutoheshimiwa kwa kipindi cha takribani miaka 40, ukiacha vifo pia yapo matokeo mengine ambayo yanaambatana na hilo.
"Kuwaweka wananchi katika hali ya woga wa kutisha ambao unaenda sambamba na wananchi kukosa imani na uwezo wa serikali yao kulinda maisha yao na mali zao, upotevu mkubwa wa maisha ya binadamu na hivyo kupunguza nguvu kazi, na wakati huo huo kuharibu sura ya nchi ndani na nje ya mipaka yake, kukua kwa misuguano baina ya wanajamii na hivyo kuondoa
amani ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ni moja ya matokeo hayo.
"Siyo sahihi kuwa juhudi zote za serikali na wadau wengine kwamba hazina nguvu, ila ni ukweli kuwa jitihada hizi hazijaratibiwa kwa kiasi cha kutosha hivyo kukosa ufuatiliaji na msukumo wa dhati wa kumaliza tatizo hilo la
mauaji," anasisitiza.
Anasema kuwa kukosekana kwa mipango fedha na nguvu baina
ya wizara na mashirika yanayohusika kukabiliana na mauaji ya wazee, aidha mauaji hayo kuchukuliwa kwa sura ya imani za kishirikina na hivyo kujenga dhana kuwa haiwezekani
kuyadhibiti pasipo shaka mahakamani kama ilivyo kwa kesi nyingine za mauaji, viongozi wa serikali, wanasiasa, na asasi za kijamii.
Kukaa kimya wakati makosa ya mauaji ya wazee yanapotokea na sera ya taifa ya wazee kutotungiwa sheria kwa miaka tisa sasa ni mojawapo ya mapungufu yanayochangia kuongezeka
kwa mauaji hayo.
"Bado tunaamini serikali ikiwaratibu kikamilifu wadau wote, pakawepo na dhamira ya dhati na uwajibikaji wa taasisi zote za serikali zinazohusika pamoja na wadau wengine tutaweza kuleta mabadiliko yatakayoondoa mauaji ya wazee nchini,".
"Vyombo vya habari vitumie nafasi yao kikamilifu kukemea kwa nguvu zote mauaji hayo na unyanyasaji wa wazee, viweza kuibua
changamoto zinazowakabili ikiwepo hili tatizo la mauaji,"anabainisha.
Anasema vyombo vya habari vifanye utetezi kuhakikisha kuwa wazee wanalindwa, kufanya ufuatiliaji kwa vyombo husika vya serikali kuhusiana na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kukomesha mauaji ya wazee.
Akifafanua katika hilo Bi. Minja anasema kuwa mfano ni
utengaji wa rasilimali zitakazowawezesha vyombo husika kushughulikia suala hili, kuhamasisha jamii kupitia taarifa mbalimbali juu ya mchango wa wazee katika ujenzi wa taifa
muhimu wa kila mwanajamii kumthamini na kulinda mzee.
Wakiungana na Bi. Minja, wazee kutoka sehemu mbalimbali
wanadai kuwa si kuuawa tu kikatili pamoja na udhalilishaji wanaofanyiwa, bali pia hata uporaji wa mali na vitisho vikubwa.
Bi. Mariam Mazinge mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, ametoa ushuhuda wake kuwa amenusurika kuuawa sambamba na kuporwa mali kwa kuwa tu ni mzee tena mjane.
"Matendo mabaya wanayofanyiwa wazee si mikoani tu bali
hata hapa Dar es Salaam na maeneo kwa mfano mengine ya
mijini, kwa mfano mimi nimekuwa nikivamiwa mara kwa mara
na kuporwa vitu vyangu, nimenusurika kuuawa...lakini
ninapokwenda katika mamlaka husika naambiwa nikamtafute
ninayemshuku badala ya polisi kuja kufanya uchunguzi
kwangu, kutokana na kupuuzwa huko kunawapa nguvu
wanaonifanyia vitendo hivyo,"analalamika.
Aidha kwa pamoja wanaitaka serikali kuacha maneno ya
kila siku kwamba wanafanya mchakato kuhusu madai ya
wazee kwani yanakwamisha hata juhudi za NGO's kufikia
malengo na hivyo utatuzi wa matatizo ya wazee kuwa ni
hadithi.
Wanaitaka serikali, katika maadhimisho ya mwaka huu
kwenda na mlolongo wa utatuzi na si hoja za baadae
ambazo zimekuwa hazina mafanikio yoyote.
Kikubwa wanataka mikakati madhubuti ya kukomesha mauaji
ya wazee na udhalilishaji juu yao, ikiwezekana
litangazwe kuwa ni janga la kitaifa ili kusaidia kumaliza matatizo hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment