02 October 2012
Tuongeze mapambano kuzuia matumizi ya dawa za kulevya
DAWA za kulevya ni kemikali ambazo huathiri ufanyaji kazi wa mfumo wa fahamu ambao unajumuisha ubongo, uti wa mgongo na kuleta mabadiliko ya hisia, fikra na tabia.
Utafiti umebaini kuwa, dawa hizo hutumiwa na watu wasiopungua milioni 155 hadi 250 duniani kote ambapo biashara ya dawa za kulevya hujumuisha upatikanaji wake na matumizi.
Shughuli hizo ni pamoja na uzalishaji, usafirishaji, mauzo, manunuzi, uhifadhi na usambazaji.
Tafiti zimebaini kuwa, waathirika wakubwa wa dawa hizo ni vijana ambao baadhi yao wamelazimika kukatisha masomo wakiwa sekondari au vyuoni pamoja na kuacha kazi.
Ukweli ni kwamba, biashara ya dawa za kulevya inakatazwa kisheria katika nchi zote duniani hivyo wahusika huifanya kwa siri pamoja na kujiunga katika mitandao mbalimbali duniani.
Katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania, kuna magenge ya watu wanaofanya biashara hii, wakati mwingine magenge hayo hupingana kimasilahi na kusababisha vita kati yao hata mbele ya jamii.
Wahusika wa mitandao hiyo husaidiana pale wanapokamatwa na kukiwa na dalili ya usaliti, mhusika hunyimwa msaada au kuuawa ambapo watu wanaofanya biashara hiyo, hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya dola ili kulinda maisha yao.
Sisi tunasema kuwa, umefika wakati wa Serikali, jamii, taasisi za Serikali na binafsi pamoja na vyombo vya dola, kukomesha biashara hii ili kuokoa maisha ya vijana ambao hivi sasa hawajishughulishi na kazi za maendeleo kutokana na afya zao kuwa dhoofu.
Wahusika wa biashara hii, huwarubuni watendaji waliopewa dhamana ya kuwadhibiti kwa kuwapa rushwa hivyo kukwamisha kasi ya mapambano yaliyopo.
Jijini Dar es Salaam, dawa hizo zinauzwa katika maeneo mbalimbali ambayo baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola, wanayafahamu lakini wanatumia fursa hiyo kupokea rushwa ili kujinufaisha.
Lengo la watendaji hao ni kujinufaisha isivyo halali wakati Taifa likiendelea kuangamia na kupoteza nguvu kazi muhimu.
Hivi karibuni, kumekuwepo na taarifa kwamba kiasi kikubwa cha dawa hizo kimekuwa kikipitishwa nchini kutoka maeneo yanayozalishwa kwenda katika masoko ya nje na kiasi fulani cha dawa hizo, hubaki nchini kwa ajili ya soko la ndani.
Ili kukabiliana na biashara hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha ushirikiano na vyombo vya dola ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Upo umuhimu mkubwa wa jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili wafanyabiashara hao wafahamike na sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment