01 October 2012

Tanzania kuiburuta Malawi mahakamani





Na Mwandishi Maalum,Newyork ,Marekani            

SERIKALI imeuambia Umoja wa Mataifa (UN) kuwa itawasilisha madai yake katika Mahakama ya Kimataifa yenye dhamana ya utatuzi wa mgogoro ili iutafutie ufumbuzi mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika ziwa nyasa.


Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, wakati akihotubia Mkutano Mkuu wa 67 UN unaoendelea nchini hapa, akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete.

"Kamwe Tanzania haitaingia vitani na Malawi katika mgogoro wa mpaka unaohusisha nchi hizi mbili katika Ziwa Nyasa badala yake itawasilisha madai yake katika Mahakama ya Kimataifa," alisema, Bw. Membe na kuongeza kuwa mahakama hiyo itakuwa mwamuzi wa mwisho wa uhalali wa mpaka huo.

Alisema Tanzania imekuwa mpatanishi mkuu wa migogoro mbalimbali duniani, ukiwemo ule wa Burundi uliokuwa ukisimamiwa na Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere na kamwe haitakuwa kielelezo kibaya cha kudai inachokiamini kwa kutumia nguvu.

"Ushiriki wa marais wetu wastaafu kuanzia Hayati Nyerere, Mhemishiwa Benjamini Mkapa na Rais Kikwete anavyohusika kutatua migogoro mbalimbali hivi sasa ni sababu tosha ya kuifanya duniani iamini kuwa njia sahihi kwa Tanzania katika kutatua mgogoro ni diplomasia, ” alisema Bw. Membe.

Kuhusu migogoro inayoendelea sehemu mbalimbali duniani, Bw.  Membe alisema kushindwa kuvumiliana kwa wanaopingana katika nyanja tofauti ni moja ya sababu ya kufanya migogoro hiyo kuzidi kushamiri na kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.

Katika mkutano huo, Bw. Membe aliiomba UN kutafuta njia ya dharura ya kutatua suluhisho la mgogoro unaoendelea nchini Syria, kati  ya majeshi ya Serikali na yale yanayompiga Rais Bashiri Alsad kutokanana na athari kubwa iliyojitokeza katika Taifa hilo hadi sasa.

"Mhemiwa wa Rais wa baraza hili wote sisi tunajua madhara ya migogoro na vita hasa pale maazimio ya Umoja wa Mataifa yanapokiukwa, hali ya Syria ni moja kati ya mifano ni vyema tukawa makini kufikiria mapema njia za kutatua migogoro kabla ya madhara kama hayo kujitokea” alisema Waziri, Bw. Membe.

Katika mkutano huo pia waziri Membe alisema Tanzania na nchi nyingine 12 zinazounda Jumuiya ya Ushirikiano Kusini mwa Bara la Afrika  SADC zimekubaliana kuunda jeshi la pamoja lenye askari 4000 kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC) kusaidia upatikanaji wa amani ya kudumu dhidi ya waasi wa M 23 wanaoipinga Serikali ya nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment