04 October 2012
TAKUKURU watoa elimu kupambana na rushwa
Na Heri Shaaban
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Wilaya ya Temeke, imetoa elimu ya kupambana na rushwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Ualimu (DUCE) ili waweze kuepuka vishawishi vya rushwa ya ngono.
Mafunzo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana na Ofisa wa TAKUKURU, wilayani humo Bi. Esther Mkokota.
Akizungumza na wanafunzi hao, Bi. Mkokota alisema tatizo la rushwa limeenea kwenye jamii nzima likiwahusisha watumishi wa Serikali na kada mbalimbali.
“Vitendo hivi vinakwamisha jitihada za maendeleo kutokana na matumizi mabaya ya madaraka, kampeni hii ni endelevu ili kutoa mafunzo kwa wanafunzi vyuoni.
“Awali tulitoa mafunzo haya kwa wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo cha Diplomasia,” alisema Bi. Mkokota na kuwataka wanafunzi kuacha kuzembea kwenye masomo wakitegemea kutoa rushwa ya pesa au ngono ili mwalimu aweze kumsaidia.
Aliwataka kuona umuhimu wa kuvaa mavazi yanayostili mwili ili kuepuka tamaa na kusisitiza kuwa, rushwa inaweza kushusha amani katika vyuo kipindi cha uchaguzi au kuchaguliwa kiongozi ambaye hakubaliki baada ya kutoa fedha au ngono.
Aliwataka wanafunzi wanapoombwa rushwa watoe taarifa katika ofisi za taasisi hiyo ili hatua staiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.
“Kuna watu ambao wanajifanya wao ni Maofisa wa TAKUKURU mitaani ili kuwadanganya wananchi, nao mkiwaona toeni taarifa waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment