01 October 2012

Serikali yaombwa kuboresha bajeti ya elimu nchini



Na Daud Magesa, Mwanza

SERIKALI imeombwa kuboresha bajeti ya elimu ili kukabiliana
na changamoto za ukosefu wa vitabu, mabaara, vifaa vyake, miundombinu ya majengo na nyumba za walimu katika shule mbalimbali nchini.

Ombi hilo limetolewa na Mhasibu wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Bw. Noel Mtekateka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Mkolani, iliyopo wilayani Nyamagana.

Kabla ya kumkaribisha Bw. Mtekateka, Mkuu wa shule hiyo, Bw. Asencio Mathias, alisema shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa walimu wa sayansi, nyumba za walimu, mabara, vifaa vyake,vitabu vya kiada na ziada na vyumba vya madarasa.

Akizungumza katika mahafali hayo, Bw. Mtekateka alisema ili
changamoto hizo ziweze kutatuliwa, Serikali haina budi kuboresha na kuongeza bajeti ya elimu pamoja na kuwaomba wadau kuisaidia sekta hiyo ambayo ni kitovu cha kuzalisha wataalamu mbalimbali.

Alisema kukosekana kwa maabara katika shule, vitabu na uhaba wa walimu, kutachangia Taifa lizalishe wataalamu wasio na uwezo.

“Shule isiyo na maabara, itasababisha Taifa likose wataalamu wa sayansi kama madaktari na wahandisi, hivyo naiomba Serikali iongeze bajeti kuboresha mazingira ya sekta hii,” alisema.

Akizungumzia mafanikio ya shule hiyo, Bw. Mathias, alisema jamii imeweza kutunza mazingira ya shule ili kuzuia mmomonyoko wa ardhi ambapo walimu na wazazi wamejitahidi kusimamia malezi ya watoto na bodi ya shule ikibaki na jukumu la kuboresha huduma.

No comments:

Post a Comment