03 October 2012

Sera za elimu zisiishie katika makabati



Na Agnes Mwaijega

ELIMU ni sekta muhimu yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa lolote duniani.

Ili sekta hii iweze kukua inategemea sera zilizowekwa kwa ajili ya kusimamia suala hilo na kuhakikisha inakuwa na mafanikio.


Ni wazi kwamba kama sera zilizowekwa hazizingatiwi na kusimamiwa ipasavyo basi sekta hiyo haiwezi kukua, kuendelea na kulipatia mabadiliko katika nyanja mbalimbali taifa husika.

Nchi nyingi zilizopiga hatua ya maendeleo duniani na kuwa na uchumi mzuri ni zile zilizojikita kuwekeza katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira kwa sababu zilitambua umuhimu wake.

Kwa sababu inaeleka wazi kwamba elimu hasa katika ulimwengu wa sasa ina umuhimu mkubwa katika kumwezesha kila binadamu kupambana na mabadiliko ya kidunia.

Lakini hii ni kinyume nchini kwa sababu sekta ya elimu haijapewa kipaumbele na kusiamamiwa ipasavyo kwa kuweka mikakati madhubuti.

Mazingira ya usomaji na ufundishaji ni magumu hasa katika maeneo ya vijijini ambapo mara nyingi utakuta madarasa ni machache ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.

Kutokana na hali hiyo kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kimekuwa kikiendelea kushuka kila mwaka hali inayoashiria mwelekeo mbaya wa elimu.

Mpaka sasa nchini bado sekta hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa sera ya elimu.

Pamoja na kwamba serikali imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kuahidi kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ikiwa ni pamoja na lengo la elimu lakini hali halisi haioneshi kama lengo hilo litafikiwa.

Hii inadhihirishwa na mapungufu mbalimbali ambayo tumekuwa tukiyaona na kuyasikia kupitia vyombo vya habari na hata ripoti za tafiti za wadau wa elimu nchini.

Ripoti hizo zimekuwa zikiibua mapungufu mazito lakini bado hatuoni hatua madhubuti zikichukuliwa.

Naamini kuwa pamoja na kuwepo kwa shule nyingi za kata zilizoanzishwa na serikali kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata elimu, lakini bado kiwango cha elimu hakiwezi kupanda kwa sababu shule hizo hazina hamasa kwa wanafunzi na hata kwa walimu.

Asilimia kubwa ya wanafunzi nchini wanasoma katika mazingira magumu hali ambayo inasababisha kiwango cha elimu kushuka.

Katika maeneo ya mengi nchini shule ziko mbali na makazi ya wanafunzi hali ambayo inasababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu na kufika shule wakiwa wamechoka.

Mfano mzuri ni hivi karibuni wakati wanafunzi wa darasa la saba wanafanya mtihani wao wa kumaliza elimu ya msingi huku wengine wakiwa wamekaa chini kwa kukosa madawati.

Mazingira ya aina hii kama mwanafunzi amekuwa nayo tangu anaanza shule yanamfanya ajisikie vibaya na kushindwa kufanya vizuri na wakati mwingine wanafunzi wengine kukatisha masomo yao.

Ni wazi kwamba kama tunahitaji kuwa na maendeleo na kutokomeza kabisa ujinga lakini kwa hali hii hatutaweza kufanikiwa kwa sababu bado hatujaweka msingi mzuri katika sekta hiyo.

Ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kuboresha mazingira ya elimu ili wanafunzi na walimu waweze kuhamsika.

Shule zote za kata ziboreshwe kwa kuwa na vifaa vyote muhimu pamoja na kujenga nyumba za walimu ili nao wakipangiwa waweze kuhamasika kwenda kufundisha hata kama shule ziko mbali.

Sera za elimu zitekelezwe kwa vitendo na sio kuishia katika makabati maofisini ili kututoa tulipo sasa.

Tutaendelea kuzalisha wataalamu wabovu bila kurekebisha mipango inayowekwa, kwa hili wadau wa elimu tushirikiane.

Kwa sababu wote tunaelewa kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha na unasaidia kuondoa ujinga na kumfanya kila binadamu kuwa mwangaza wa maisha.

0717157517





No comments:

Post a Comment