02 October 2012

RT yaridhishwa maandalizi Rock City


Na Mwali Ibrahim

CHAMA cha Riadha Tanzania (RT), kimeridhishwa na maandalizi ya mwaka huu ya mbio za Rock City Marathon, zitakazofanyika Oktoba 28 mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema amekuwa akifanyakazi za maandalizi na waandaji wa mbio hizo pamoja na Chama cha Riadha Mwanza kuhakikisha mbio za mwaka huu zinafana kuliko za mwaka jana.

Mbio hizo kauli mbiu yake ni 'tukuze utalii wa ndani kupitia michezo'.

"Sisi kama Chama cha Riadha, tunajivunia kuona kwamba maandalizi ya Rock City Marathon mwaka huu yanaendelea vizuri na tunaipongeza Kampuni ya Capital Plus International (CPI), kuandaa mbio hizi vizuri kila mwaka.

"Kupitia tamasha hili kunasaidia kukuza vipaji vipya katika riadha na inasaidia pia kupata wanariadha wazuri, ambao wanaweza kuitangaza nchi katika mataifa mbalimbali," alisema.

Nyambui alisema mashindano hayo yanashirikisha wanariadha wa nchi jirani, ambao baadhi yao tayari wamethibitisha kushiriki.

Alisema kwa kuchuana na wanariadha wa hapa nchini kunazidi kuwaongeza uwezo wanariadha na hata kuwapa hamasa ya kutaka kufikia viwango vikubwa kimataifa.

Naye Mratibu wa mbio, Grace Sanga alisema washiriki wategemee ushindani mzuri zaidi kutokana na maandalizi yaliyoanza kufanywa mapema kwa kushirikiana na RT pamoja na wadhamini.

Aliwataja wadhamini wa mashindano hayo kuwa ni NSSF, Airtel, PPF, Geita Gold Mine, African Barrick Gold, ATCL, TANAPA, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nyanza Bottles, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.

No comments:

Post a Comment