02 October 2012
Kayumba mabingwa wapya wa pool
Na Mwandishi wetu, Mwanza
TIMU ya pool ya Kayumba kutoka Mkoa wa kimichezo wa Ilala jijini Dar es salaam, juzi ilitawazwa kuwa mabingwa wapya wa taifa wa mashindano ya 'Safari Lager National Pool Championship 2012', baada ya kuikung'uta Meeda ya Kinondoni magoli 13-2 katika mchezo wa fainali.
Fainali hizo ambazo zilishirikisha timu 16 ambazo zilikuwa mabingwa kwenye mikoa yao katika mashindano ngazi ya mikoa, zilifanyikia kwenye Ukumbi wa hoteli ya Monarch jijini hapa na kudhaminiwa na wadhamini Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safri Lager.
Kayumba kwa kutwaa ubingwa huo walizawadiwa fedha sh. milioni tano, kombe la ubingwa na medali za dhahabu.
Meeda wenyewe kwa kushika nafasi ya pili waliondoka na fedha taslimu sh. milioni 2.5, 2eyes ya Arusha iliyoshika nafasi ya tatu ilijinyakulia sh. 1,250,000 na Anatory ya Morogoro iliyoshika nafasi ya nne ilipewa sh .750,000.
Kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume), bingwa wa Mkoa wa Mbeya, Solomon Elias ambaye ni bubu alitwaa ubingwa huo wa taifa baada ya kumkandamiza, Athuman Selemani wa Morogoro magoli 5-1 katika mchezo wa fainali na kujinyakulia sh. 500,000.
Athumani Selemani kwa kushika nafasi ya pili alizawadiwa sh. 250,000, wakati Fayuu Staniley wa Arusha alipewa sh. 200,000 kwa kushika nafasi ya tatu huku Ally Nada wa Manyara aliyeshika nafasi ya nne aliambulia sh. 150,000.
Mkoa wa Mbeya upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanawake) Betty Sanga naye alitwaa ubingwa wa taifa wa mashindano hayo, baada ya kumchapa Cecilia Kileo wa Kilimanjaro magoli 5-2 katika mchezo wa fainali.
Betty kwa kutwaa ubingwa huo alijinyakulia fedha sh. 350,000, wakati Cecilia aliyeshika nafasi ya pili aliondoka na sh. 200,000, Sada Tulla wa Shinyanga aliyemaliza fainali hizo akiwa nafasi ya tatu alizawadiwa sh. 150,000 na Anna wa Iringa aliyeshika nafasi ya nne alipewa sh. 100,000.
Zawadi zote kwa washindi zilikabidhiwa na Mkurugenzi wa Michezo Tanzania, Leonard Thadeo ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele cha fainali hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment