03 October 2012

Petroli, dizeli zashuka bei *EWURA: Wanunuzi ombeni stakabadhi


Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), jana imetoa bei kikomo za mafuta ya petroli na dizeli ambazo zitaanza kutumika kuanzia leo nchini kote.

Lita moja ya mafuta ya petroli imeshuka kwa sh. 306, wakati dizeli imeshuka kwa sh. 192 ambapo bei ya mafuta ya taa haijabadilika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo, bei ya mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam itakuwa sh. 1,994, kwa lita moja wakati bei ya awali ilikuwa sh. 2,300.

Mafuta ya dizeli imeshuka na kufikia sh. 1,950 kutoka sh. 2,142, wakati mafuta ya taa yakibakia sh. 1,993 kwa lita moja kwa sababu hakuna meli yoyote iliyoingia nchini.

Bw. Kaguo aliongeza kuwa, bei hizo zitaendelea kuongezeka kutokana na gharama za usafirishaji kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, ingawa katika kila eneo punguzo litakuwa ni sh. 306 kwa lita moja ya petroli na dizeli sh. 192.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta mwaka 2008, alisema bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.

Aliongeza kuwa, lengo ni kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta kulingana na bei anayoiona mteja inamfaa.

“Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo na kama mfanyabiashara atakiuka atapewa adhabu ya kulipa sh. milioni tatu,” alisema Bw. Kaguo.

Alivitaka vituo vyote kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana ili kumfanya mteja afanye uchaguzi wa kununua mafuta akiwa anajua bei halisi katika kituo husika.

“Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta ambayo yamenunuliwa na bei kwa lita.

“Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha ununuzi wa mafuta kama kutatokea malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au mteja kuuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa,” alisema.


No comments:

Post a Comment