03 October 2012

CCM yazidi kumuandama Dkt. Slaa



Na Mwanajuma Juma, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, kuacha kukipigia ramli chama chao.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Bw. Issa Haji Usi Gavu, aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Alimtaka afanye utafiti zaidi ili kujua nguvu ya chama hicho kisiasa ndio maana wananchi wanakipa ushindi katika chaguzi mbalimbali.

Bw. Gavu alisaema Dkt. Slaa hana kigezo kinachothibitisha CCM imekufa au itakufa na kumtaka atambue kuwa, nguvu ya chama hicho kisiasa ni kubwa na haizuiliki kwa maneno ya kujifariji.

“Apite kuanzia Ileje hadi Kisiwapanza, aanzie Kamachumu hadi
mkokotoni, ataona joto la CCM lilivyotanda, huu ni uhai sio kifo kama anavyosema ili kuwadanganya Watanzani,” alisema.

Akizungumzi sakata la kudondoka kwa baadhi ya vigogo wa chama hicho wakiwemo wabunge, wawakilishi na makada maarufu kwenye chaguzi za chama hicho, Bw. Gavu alisema hali hiyo si sehemu ya utekelezaji mpango wa kujivua gamba.


“Matokeo ya chaguzi zinazoendelea hayana uhusiano wowote na kuanguka kwa baadhi ya vigogo katika chaguzi zinazoendelea bali
ni matokeo ya kawaida yanayotoa tafsiri ya demokrasia kuchukua mkondo wake,” alisema.

Bw. Gavu aliongeza kuwa, matokeo ya chaguzi za CCM yatasaidia kuimarisha uhai wa chama hicho na wanafurahi kupata viongozi wapya wenye upeo, ufahamu na wanataaluma.

“Chama chetu kimepiga hatua katika suala zima la demokrasia kwa kuwa na mtazamo mpya, wanachama wetu ni wakomavu, tumepata safu ya viongozi ambao wataheshimu, kufuata maadili na wazalendo watakaojitenga na vitendo vya rushwa na ufisadi,” alisema.

Aliongeza kuwa, chaguzi hizo ni muhimu kwa uhai na maendeleo ya chama hicho na umeonesha dira ya mabadiliko na ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumza kwa kujiamini, Bw. Gavu alisema chaguzi hizo zimezingatia kanuni na taratibu hivyo wagombea ambao wataambulia patupu, wanayo nafasi ya kushiriki tena katika uchaguzi ujao ifikapo 2017.

No comments:

Post a Comment