08 October 2012
Niwasomee nini wakati hakuna vyanzo vya mapato-Mwenyekiti
Na David John
SIKU chache baada ya wananchi wa Mtaa wa Kivule Kitunda Wilayani Ilala kumtaka Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw.Joseph Gasaya kusoma taarifa ya mapato na matumizi na kudai kuwa tangu ashike nafasi hiyo hajawahi kutoa taarifa yeyote kwa wananchi wake.
Mwenyekiti huyo amejibu mapigo na kudai kuwa hawezi kusoma taarifa ya mapato na matumizi, kwani katika mtaa wake hakuna vyanzo vyovyote vya mapato ama miradi ambavyo vinamlazimisha atoe taarifa kwa wananchi.
Akizungumza na Gazeti hili Dar es salaam jana katika ofisi za mtaa huo Bw. Gasaya alisema anashangazwa na hatua ya wananchi hao kudai kusomewa taarifa ya mapato na matumizi wakati katika mtaa huo hakuna mradi wala kitu chochote cha kuingiza fedha.
Alisema wananchi wanatakiwa watambue kuwa yeye ni Mwenyekiti wa serikali ya mtaa na siyo kijiji hivyo anayesitahili kutoa taarifa ya mapato na matumizi ni ofisi ya kata ambayo ipo chini ya Diwani na si vinginevyo.
Alisema Diwani yeye anapata ruzuku kutoka serikalini yaani kupitia halmashauri hivyo anasitahili kutoa taarifa kwa wananchi katika kile kinachofanyika kupitia fungu lile ambalo limetoka kwa ajili ya maendeleo ya kata husika lakini siyo mtaa.
"Nawashauri wananchi kwamba kama wanataka kujua taarifa hizo basi nikupitia ofisi ya serikali ya kijiji ama kata na siyo serikali ya mtaa kwani sisi hatuna vyanzo vya mapato,"alisema
Aliongeza kuwa wananchi kama hawataki kukubaliana na maneno yake basi waende katika ofisi ya Mkurugenzi wakaulize kama kuna ruzuku yeyote inatolewa kwa ajili ya kuendeshea mitaa na siyo kuleta malalamiko ambayo hayana tija.
Katika hatua nyingine Bw. Gasaya aliwaomba wananchi wake kufuata taratibu na kanuni zilizopo na siyo kutoa vitisho ambavyo kimsingi havina mbele wala nyuma.
"Kama kuna madai ya msingi kuhusu ofisi yake ni vema wananchi wakajenga tabia ya kuja ofisini kwangu ili kujirizisha kuhusiana na mambo yanayolalamikiwa na siyo kusemea pembeni na kutoa vitisho ,kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa ."alisema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment