05 October 2012
Nishati mbadala kunusuru misitu yaonesha mafanikio
Na Rose Itono
TAFITI mbalimbali zimekuwa zinafanywa na wataalamu wengi katika nyanja tofauti za kiuchumi ili kuona ni kwa namna gani mwananchi anaweza kujikomboa na umaskini.
Ukipitia tafiti hizo utabaini kuwa yapo mambo mengi ambayo yanakosekana kwa walengwa kufikia malengo wanayojiwekea.
Lipo suala la mitaji ya fedha, teknolojia ya kufanyia uzalishaji wao, masoko ya kuuza bidhaa zinazozalishwa pamoja na elimu ndogo ya ujasiriamali ya kutambua ni biashara ya aina gani inaweza kufanyika, wakati gani na mahali gani.
Kutokana na hali hiyo Kampuni ya Arti Tanzania inayojishughulisha na nishati mbadala ilianzisha mradi wa kutengeneza mkaa mbadala unaotumia mimea mikavu ya shambani ili kuwezesha kupunguza uharibifu wa misitu unaotokana na ukataji miti ovyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Bw.Nachiket Potnis anasema kutokana na hali hiyo kampuni yake ilianzisha mradi wa kutengeneza mkaa mbadala kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Anasema mradi huo uliwezesha kufunguliwa kwa kiwanda cha Brikwiti Company kilichopo Bagamoyo mkoa wa Pwani kuandaa mkakati wa kuhakikisha wanashirikisha jamii hasa vijijini ili kupeana ujuzi wa namna ya kutengeneza mkaa mbadala.
Anasema elimu hii iliwawezesha baadhi ya watu kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kujipatia vipato na pia ilisaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa umuhimu wa matumizi ya mkaa huu kwa kuwa umesaidia kupunguza uharibifu wa misitu.
Anasema kupatikana kiwanda hicho baadhi ya wananchi wa Bagamoyo na Kibaha waliweza kupata ajira na kuwa wawezeshaji kwa wananchi wengine.
Anaongeza kuwa, kutokana na upya wa teknolojia hii ya mkaa mbadala walianzisha mpango kwa kuhakikisha wanawapa elimu wananchi vijijini ili waweze kuwa wajasiriamali.
Bw. Potnis anasema elimu ya utengenezaji wa mkaa bila kuharibu mazingira kwa kutumia mimea mikavu na mabaki ya shamba yanayotokana na kilimo umewezesha kupunguza ukataji miti ovyo na kuchoma mikaa.
Mkurugenzi anasema kukosekana kwa mitaji teknolojia ya kufanyia uzalishaji na masoko ya kuuzia bidhaa wanazozalisha iliamua kutoa mafunzo kwa wananchi vijijini ili waweze kuinua uchumi.
Anasema kampuni hiyo imeanza mwaka 2007 ikiwa na lengo la kutafuta teknolojia muafaka na kuisambaza kwa jamii hasa vijijini ili waweze kuongeza pato.
Anasema mwaka 2009 kampuni hiyo ilishinda tenda iliyotangazwa na Benki ya Dunia kwa kuandika mchanganuo kuhusu namna ya kuhudumia kwa kutumia mimea mikavu.
Kutokana na kushinda tenda ilianza kutoa elimu katika vijiji 24 kwenye wilaya mbili za Kibaha na Bagamoyo kuhusu utengenezaji wa mkaa mbadala unaotumia mabaki ya shamba yanayotokana na kilimo au mimea mingine mikavu.
Bw.Potnis anasema zaidi ya wananchi 1000 kwenye wilaya hizo walipatiwa elimu hiyo na vifaa ili kuwawezesha kufanya kazi kwa vitendo.
Anasema baada ya kumaliza elimu yao wanavijiji waliunga vikundi ili kuwawezesha kuzalisha kwa pamoja na kujipatia kipato.
Kutokana na hali hiyo wanakijiji hao wameweza kujipatia kipato kwa kuwekeza kwa asilimia 30 kwenye kampuni ya Art Tanzania kupitia kiwanda chake cha kutengeneza mkaa mbadala unaotumia mimea mikavu kwa kukusanya vumbi linalotokana na mimea hiyo kwa kutumia mashine maalumu walizopatiwa baada ya mafunzo na kuuza kwenye kampuni hiyo.
Naye Meneja mradi wa Kampuni ya Brikwiti (BBC) Bw.Allan Shaidi anasema wamejiandaa kutoa elimu kwa vijiji vingine mwakani ili kupanua wigo wa upatikanaji wa vumbi la mimea kwa kiwanda kwa ajili ya kupata mkaa wa kutosha.
Anasema baada ya mafunzo hayo wanatarajia kuanzisha vikundi vingine ambavyo vitanufaika kama vile vya awali kuwa wawekezaji katika kampuni yao na kupata asilimia 30 ya pato linalopatikana.
Anazungumzia kuhusu mkaa huo anasema mkaa mbadala ni rafiki wa mazingira, unatokana na asili ya mimea mikavu, hivyo ni mkaa na unaweza kuwashwa na kukolezwa sawasawa na mkaa wa kawaida.
Bw. Shaidi anasema mkaa huo unaweza kupunguza gharama kubwa kwa watumiaji kwani unaweza kuendelea kuwaka kwa saa moja hadi moja na nusu baada ya kuwashwa.
Anasema unaweza kuutumia na majiko yoyote ya kawaida, lakini siku hizi kuna majiko yanayoohifadhi moto vizuri zaidi hivyo huokoa pesa zako kwa asilimia kubwa.
Anaitaka serikali na jamii kuunga mkono utumiaji wa mkaa mbadala kwani ni rafiki wa mazingira, huokoa pato na miti yetu ambayo ndiyo vyanzo vya maji ya sasa na vizazi vinavyotufuatia.
Kwa upande wake msimamizi wa Kiwanda hicho mjini Bagamoyo Bw.Yasin Thabit anasema ni vema serikali ikalipa kipaumbele suala la teknolojia mbadala ili kupunguza ukame unaosababishwa na ukataji wa miti.
Anasema kuungwa mkono kwa teknolojia hii kutaiwezesha sura ya nchi kuwa nzuri kwa kuokoa misitu na vyanzo vya maji na pia kutawezesha jamii kujipatia ajira kuwa wajasiriamali.
Anaongeza kuitaka jamii kutumia fursa zinazopatikana kwa kuhakikisha wanainua uchumi wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment