08 October 2012

Nashangaa Halmashauri kukataa madai ya walimu Lindi -Oluoch


Na Thureya Dabas

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Bw. Ezekiah Oluoch ameshangazwa na kitendo cha halmashauri ya lindi vijijini kukataa madai ya walimu walioko Lindi.

Akizungumza na mwandishi kwa njia ya simu jana, Bw. Oluoch alisema kuwa kwa taarifa walizonazo mpaka sasa ni walimu wa Lindi vijijini ambao wamekatwa madai yao kutokana na sababu zisizojulikana.

"Sisi kama chama cha walimu hatua tuliochukuwa mpaka sasa ni kumuandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lindi vijijini ili kujua chanzo cha walimu hao kukatwa madai yao,"alisema.

Alisema kuwa amesikitishwa na hatua ya Mkurungezi huyo kukata madai ya walimu kwa sababu zisizojulikana na kuongeza kuwa walimu walio wengi wanaishi kwenye mazingira magumu kutokana na kipato duni.

Aidha alisema kuwa Mkurungenzi huyo alipaswa kuwa mstari wa mbele katika kupigania madai ya walimu na sio kukata kwasababu wanategemea kuendesha maisha na familia zao.

"Walimu wenyewe bado wana maslahi duni badala ya kupambana na kile kidogo wanachopata, lakini utashangaa baadhi ya walimu wanakatwa madai yao pasipo sababu zinazojulikana,"alisema.

Aliongeza kuwa wao kama CWT wanasubiri wapate majibu kutoka kwa Mkurugenzi huyo ambapo pia wanahitaji awape majibu ikiwa ni pamoja na orodha ya majina ya walimu hao na kiasi ambacho wamekatwa ili waweze kufuatilia kwa umakini zaidi.








No comments:

Post a Comment