05 October 2012

'Mfumo wa elimu uandaliwe upya kuhimili mabadiliko'


Na Daniel Samson

ELIMU ni nyenzo muhimu ya maendeleo inayotolewa katika mfumo rasmi ambao hujumuisha malengo ili kutekeleza sera za nchi
katika kuboresha maisha ya jamii.


Mjadala umeibuka kwa wadau wa elimu kuhusu hali ya elimu nchini na mstakabali wake ili kumaliza changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Hali  hiyo imejitokeza wakati huu kwa sababu ufaulu wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari unashuka kila mwaka na kuacha maswali mengi kwa watu.

Kiini cha malumbano ni mabadiliko hasi yanayotokea katika sekta hii ikilinganishwa na kipindi cha utekelezaji wa sera za ujamaa ambapo elimu inatajwa kuwa bora.

Swali wanalojiuliza wengi ni kwa nini elimu inayotolewa wakati huu haina thamani kuliko iliyotolewa wakati wa mfumo wa ujamaa katika awamu ya kwanza na ya pili ya utawala wa nchi hii.

Hapa ndipo mkanganyiko unapoibuka na kuacha maswali mengi yasiyo na majibu hata kwa watunga sera.

Kigezo cha kupima ubora wa elimu sio sahihi katika kulinganisha mfumo wa elimu uliotolewa wakati huo na sasa  katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Tunapolinganisha ufanisi wa elimu katika kipindi cha ujamaa na wakati huu ambao tunaongozwa na sera za kibepari tuwe na vigezo halisi ambavyo vitatusaidia kupata jibu la kwa nini elimu yetu inakabiliwa na changamoto zilizokosa suluhisho.

Tukiendelea kulaumiana na kuchukiana juu ya elimu inayotolewa sasa tutakuwa tunafanya makosa kwa kuwapatia ujuzi usio na manufaa kwa maisha yao ya baadaye.

Malengo tuliyonayo katika mfumo wa elimu ya sasa yanaweza kutusaidia kutafuta mwarobaini wa kufeli kwa wanafunzi na kupungua kwa ubora wa elimu Tanzania.

Malengo sio lazima yaandikwe katika vitabu lakini hali halisi ya elimu inadhihirisha wazi kwa sababu serikali inaongozwa na wanasiasa ambao wana ushawishi mkubwa katika shughuli za serikali ambapo ndio huamua elimu iwe katika mfumo upi ili kutimiza maslahi yao.

Elimu ya Tanzania imepitia vipindi vitatu tofauti ambavyo vya mfumo tofauti wa utawala kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo huitaji mfumo rasmi wa elimu ambao utatimiza malengo yanayokusudiwa.

Katika kipindi cha ukoloni, malengo ya elimu yalikuwa ni kuwaandaa wahitimu katika nyanja za uongozi na uchumi ili kutumikia serikali za watawala wa Kijerumani na Waingereza.

Wasomi walifundishwa tamaduni za kigeni ambazo zililenga kudhohofisha mila na desturi za Afrika. Elimu iliyotolewa ilikuwa na viwango kwa sababu ililenga watu wachache ambao
waliandaliwa kuwa viongozi ambao walitumikia serikali na  kutekeleza sera za kikoloni kwa waafrika wengine ambao hawakutaka kuongozwa na wakoloni.

Pia ilikusudia kutoa stadi muhimu za maisha kama ushonaji, ufundi seremala na washi. Waliopata stadi hizi walifanya kazi ya kujenga makazi ya watawala wa kizungu, miundombinu
ya barabara na reli ambayo ilitumika kusafirisha malighafi kwenda viwandani.

Utafiti unaonyesha kuwa, elimu hii ilikuwa na malengo yaliyokamilika kwa sababu ilizingatia mahitaji muhimu ya wakoloni walipotawala Tanganyika.

Baada ya uhuru na nchi kuingia katika mfumo wa ujamaa, serikali ndio ilikuwa na jukumu la kutoa huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo elimu kuanzia awali hadi chuo kikuu. Lengo kuu likiwa likuwa ni kuwaandaa vijana ambao walipewa taaluma mbalimbali ambazo ziliendana na mahitaji ya jamii kwa wakati huo.

Wanafunzi waliandaliwa kuwa wazalendo ambao waliipenda nchi yao na taaluma walizopata zilitumiwa kuendeleza rasilimali za nchi ili kujiletea maendeleo kwa sababu taifa kwa wakati huo lilikuwa changa na lilihitaji nguvu ya pamoja ya kutumia utajiri wa nchi kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa bila
kujali matabaka yaliyokuwepo katika jamii.

Taifa lilikuwa na watu wachache ikilinganishwa na idadi ya watu iliyopo sasa ambayo inafikia watu milioni 43, hata idadi ya wanafunzi waliojiunga na shule za msingi na sekondari ilikuwa ndogo kwa sababu serikali iliendelea kutumia sera na mitaala ya wakoloni.

Sera hiyo ililenga watu wachache kupata elimu katika miundombinu na mazingira rafiki yaliyosaidia kwa asilimia kubwa wanafunzi kusoma na kuhitimu wakiwa na uwezo na ujuzi mkubwa kufanya kazi na kuleta matokeo chanya katika uchumi wa nchi.

Serikali ilitambua umuhimu wa elimu na mchango wake katika maendeleo ya taifa iliweka mipango na sera ambazo ziliifanya elimu kuwa bora zaidi.

Mwanafunzi aliyehitimu darasa la saba alikuwa na maarifa na  stadi muhimu ambazo zilimwezesha kujiajiri mwenyewe lakini ni tofauti na kipindi hiki ambapo wakihitimu hawawezi kujiajiri na kujenga maisha yao kutokana na elimu inayotolewa kuwa ya nadharia zaidi kuliko vitendo ikihusisha mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanayotokea nchini.

Malengo yaliyowekwa ndio yaliyoifikisha elimu katika kiwango bora ambacho wengi wanaamini kuwa kilikuwa cha kuridhisha kutokana na matunda yaliyopatikana.

Katika hili hatupaswi kulaumu na kutamani kurudi katika mfumo wa zamani kwani kila zama zina malengo yake.

Malengo yaliyopo katika mfumo wa kibepari ambao nchi inatawaliwa nao huwezi kutumia mfumo huo wa zamani kufanikisha malengo ya wakati huu.

Jukumu la kutoa huduma za jamii ikiwemo elimu sio la serikali pekee bali linahusisha watu binafsi kuanzisha taasisi za elimu kwa sababu mfumo wa kibepari unatoa uhuru kwa kila mtu kutimiza majukumu yake bila kuingiliwa na serikali.

Kutokana na mgawanyo huu wa elimu, shule binafsi zimeonekana kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa sababu wamiliki wake wanatoa elimu bora ambayo inazingatia
mahitaji yote ya shule.

Hata hivyo elimu inayotolewa wakati huu ina mkanganyiko mkubwa ambapo kujua hasa  ina malengo gani na mstakabali kwa taifa. Elimu ni taaluma lakini siasa imeingia katika elimu na hivyo utekelezaji wa sera na mipango ya elimu inategemea matakwa ya wanasiasa waliopo madarakani  ambao wana ushawishi mkubwa katika shughuli za jamii.

Elimu inayotolewa ina muktadha wa ubinafsi ambao unamfanya mhitimu kujiajiri maisha yake na kusahau mchango wake katika jamii.

Wanafunzi wengi leo wanawaza  kuajiriwa katika ofisi za mashirika makubwa na serikalini ili kujilimbikizia mali nyingi na kuwa matajiri kwa mda mfupi bila kutumia
uwezo walionao kutumia rasilimali za nchi kuleta maendeleo katika taifa.

Uwajibikaji wa viongozi katika elimu umepungua na hili
linafanyika kwa makusudi ingawa haliko wazi kwa sababu wanasiasa wanatunga sera nzuri lakini hazitekelezeki na kuiacha sekta ya elimu ikiyumba na kukosa ufumbuzi wa matatizo yaliyopo katika sekta hii.

Ikiwa serikali inashindwa kuboresha maslahi na mazingira ya walimu huku ikitumia rasilamali nyingi kusomesha walimu ili wakawafundishe wanafunzi, lakini kama mazingira ya kufanyia kazi kwa walimu kama hayataboreshwa tutaendelea kupiga kelele na kuwalaumu walimu kuwa hawatekelezi wajibu wao.

Kama unajenga shule nyingi na kudahili wanafunzi wengi ambao wengine hawajui kusoma na kuandika katika shule za kata, na kujisifu kuwa umeboresha elimu na kuongeza idadi ya wanafunzi lakini shule hizo hazina vifaa vya kufundishia na kusomea, miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi.

Ndio maana ninasema siasa imeingia katika elimu na wananchi
wanadanganywa kwa kuhimizwa kuwapeleka watoto shuleni ambao wakifanya mitihani ya kitaifa hufeli kuliko wanaofaulu.

Haya ndio malengo ya elimu inayotolewa wakati huu, tutafakari na kuhoji nini mstakabali wa elimu yetu kwa miaka mitano ijayo, je tutafika ikiwa wanafunzi wanaenda shule lakini hawana walimu wa kuwafundisha.

Kundi linalotawala kundi kubwa linafanya makusudi kurudisha elimu nyuma ili kulinda maslahi binafsi ya kutawala kwa sababu watu wakielimika watatoka katika umaskini wa fikra na
kuanzisha harakati za kuleta maendeleo nchini.

Elimu yetu inahitaji mabadiliko makubwa ya mfumo wa kisiasa ambao utaifanya sekta ya elimu kuwa taaluma inayojitegemea.

No comments:

Post a Comment