08 October 2012
Kinondoni waanza kubomoa nyumba za mabondeni Dar
Na Agnes Mwaijega
MANISPAA ya Kinondoni imeanza kutekeleza mpango wa kubomoa nyumba zote zilizojengwa katika maeneo ya bondeni.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na serikali kuwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuondoka na kwenda kwenye viwanja walivyopewa katika eneo la Mabwepande.
Akizungumza na Gazeti hili Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Bw.Sebastian Mhovella alisema mpango huo ambao umeanza kwa kubomoa nyumba zaidi ya 130 katika eneo la Hananasifu,serikali ndiyo imeruhusu ili kuhakikisha kwamba wananchi wote wa mabondeni wanaondoka kabla mvua hazijaanza kunyesha.
"Bomoabomoa iliyoanza jana ni mkakati madhubuti wa serikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wanaoishi mabondeni wanaepukana na athari za mafuriko," alisema.
Alisisitiza kuwa katika zoezi hilo ambalo limeanza jana asubuhi jumla ya nyumba 217 katika maeneo ya Hananasifu na Sunna zitabomolewa.
Bw.Mhovella aliongeza kuwa wananchi hao tayari walishapewa viwanja muda mrefu Mwabepande ili waweze kwenda kujenga makazi yao.
Alisema katika zoezi hilo manispaa itabomoa nyumba zote zilizoko kwenye maeneo yote ya bondeni ili kuwanusuru wananchi hao na athari za mvua na mafuriko.
Majira ilifika eneo la tukio na kujionea jinsi zoezi hilo linavyoendelea huku wakazi wa eneo hilo wakihangaika kubeba vitu vyao ili kupisha zoezi hilo.
Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)ilitoa taarifa kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mvua kunyesha na hivyo kutoa agizo kwa wananchi wanaoishi mabondeni kuanza kuondoka mapema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment