05 October 2012

Jina langu linatumika kutapeli- Mulugo


Na Anneth Kagenda

ZIARA za kushtukiza zinazofanywa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo, zimeanza kumtokea puani baada ya watu wasiofahamika kutumia jina lake kujipatia fedha kwa njia ya utapeli.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Mulugo alisema matapeli wameanza kutumia jina lake vibaya tangu aanze ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za elimu nchini.

Alisema tabia ya watu kutumia jina lake kutapeli ilianza taratibu, lakini hivi sasa imezidi kushika kasi ambapo jana tapeli mmoja alimpigia simu Mhasibu wa Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) na kumweleza Bw. Mulugo amemtuma sh. milioni 1.5.

“Ndugu zangu waandishi, naomba mnisaidie katika hili, kuna namba imepiga leo (jana), kwa Mhasibu wa TEA, kutaka sh. milioni 1.5 akitumia jina langu, tukio la aina hii pia limetokea katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoani,” alisema na kuongeza kuwa chanzo cha tatizo hilo ni ziara zake za kushtukiza.

Alisema wengine wamekuwa wakipiga simu na kuomba kiasi cha fedha wakidai Bw. Mulugo anataka kukitumia kwa ajili ya mafuta
ya gari lake ili aweze kufanya kazi za Serikali kwa ufanisi.

“Mimi nikitaka kufanya ziara huwa simfahamishi mtu labda bosi wangu Waziri (Dkt. Shukuru Kawambwa), nawaonya Wakurugenzi, Maofisa Elimu wa mikoa, Wilaya na wadau wa elimu waache kutumia jina langu vibaya kwani wakibainika sheria itachukua mkondo wake,” alisema Bw. Mulugo.

Alitoa mfano kama Mhasibu wa TEA asingepita ofisi kwake
kujiridhisha kama kweli anahitaji fedha hizo, fedha hizo zingeangukia mikononi mwa matapeli.

Akizungumzia mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Jumatatu, Bw. Mulugo alisema yeyote atakayejihusisha na vitendo vya wizi wa mitihani adhabu kali zitachukuliwa.

“Tumejipanga vizuri katika hili, hadi sasa hakuna mahali ambapo kuna taarifa za mtihani kuvuja, atakayesababisha kuwapo kwa
dosari yoyote, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.


No comments:

Post a Comment