04 October 2012

Jamii ijifunze lugha ya alama-CHAVITA



Na Mariam Mziwanda

CHAMA cha Viziwi Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, (CHAVITA), kimeiomba jamii ijifunze lugha ya alama kupunguza unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

Katibu wa chama hicho, Bw. Juma Abdul, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika semina mafunzo ya utawala bora ambayo yalishirikisha watu wenye ulemavu huo wilayani humo.

“Ipo haja ya jamii na watoa huduma kujifunza lugha ya alama kwani tunashindwa kupata huduma stahiki tunapokwenda hospitali, polisi na maeneo mengine kwa sababu ya ukosefu wa wakalimani.

“Jamii ikijifunza lugha hii, itatoa fursa sawa kwa viziwi kujifunza mambo mbalimbali pamoja na sera ya utawala bora ambayo wengi hawaifahamu vya kutosha,” alisema.

Alisema elimu inayotolewa katika mafunzo hayo itawasaidia wanachama na viongozi wa CHAVITA kuelewa majukumu yao kwani tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2005, hawajawahi kupata mafunzo kama hayo.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya waitakayo na kudai kuwepo kwa fursa sawa.

No comments:

Post a Comment