05 October 2012

CWT KUSUSIA MAADHIMISHO SIKU YS WALIMU

Na Darlin Said

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimetangaza kutoshiriki katika maadhimisho ya siku ya walimu yanayofanyika leo duniani kote, kwa madai kuwa Serikali imeshindwa kutimiza madai yao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa CWT Bw.Gratian Mukoba, alisema na badala yake walimu wataadhimisha siku hiyo, wakiwa kazini wamekata tamaa.

Bw Mukoba alisema lengo la maadhimisho hayo ni kutathmini kile walichofanyiwa na mwajiri wao, lakini kwa upande wao hawana cha kukumbuka zaidi ya kuwa na majonzi.

"Serikali imefanya maamuzi ya kisiasa kwa kutowekeza ipasavyo kwenye sekta ya elimu kutokana na kuwekeza kwa kiasi kidogo cha asilimia 1.4 ya pato la taifa.

"Hivyo Tanzania ndiyo inayoongoza katika kuwalipa mashahara duni ikilinganishwa na nchi za Afrika Mashariki ambao haukidhi mahitaji ya walimu hali inayopelekea kutoheshimiwa na jamii kama wafanyakazi"alisema Bw.Mukoba.

Hata hivyo ametoa wito kwa serikali kukubali kurudi katika meza ya majadiliano ya pamjoa na chama hicho  na iwalipe madeni wanayodaiwa na walimu, wakufunzi pamoja na wakaguzi wa shule.

Naye Katibu wa CWT Bw.Ezekiel Oluoch alisema Serikali imegoma kukutana na CWT kama ilivyoagizwa na mahakama na Bunge ingawaje tayari tumeshawandikia barua  ya  kukutana nao kwa mazungumzo lakini mpaka leo hawajajibu .
 
Sambamba na hilo Bw.Oluoch aliwataka  watanzania na jumuiya ya kimataifa kujitokeza kuwatetea walimu dhidi ya kile walichokidai  manynyaso wanayopata kutokana na mishahara duni isiyokidhi mahitaji muhimu ya kila siku.

No comments:

Post a Comment