03 October 2012

AJALI MBAYA MBALIZI Mbunge CCM anusurika kufa *Ni Dkt. Mary Mwanjelwa, Katibu wake ateketea moto *Watu zaidi ya nane wahofiwa kufa, imehusisha magari 4 *Basi la Dar Express nalo laungua moto, 48 wanusurika


Charles Mwakipesile na Esther Macha, Mbeya

MBUNGE wa Viti Maalumu, mkoani Mbeya, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Mary Mwanjelwa, amenusurika kufa katika ajali mbaya iliyotokea jana eneo la Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Vijijini baada ya gari lake kugongwa na kuteketea kwa moto.

Habari zilizotufikia wakati tukienda mtamboni zinadai kuwa, ajali hiyo imehusisha magari manne likiwemo lori la mafuta ambalo linamilikiwa na Kampuni ya Lake Oil, lenye namba T 814 BTC,
gari ndogo ya abiria (hiace), yenye namba  T 299 BCE na gari ya Mbunge huyo aina ya Toyota Hilux, namba T 671 ABM.

Inadaiwa kuwa, zaidi ya watu nane walifariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa kutokana na mlipuko mkubwa wa moto uliotokea baada ya gari hizo kugongana.

Mashuhuda wa ajali hiyo wakiwemo majeruhi, walisema lori lililokuwa limebeba mafuta, lilifeli breki katika mteremko mkali wa Mlima Iwambi hivyo kuliparamia lori lingine na kuigonga gari ya Dkt. Mwanjelwa kisha kuvaana uso kwa uso na gari ya abiria iliyokuwa ikitokea eneo la Mbalizi.

Kutokana na ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Abbas Kandoro alifika eneo la tukio, kutoa pole kwa wafiwa na kwenda Hospitali ya Ifisi Mbalizi kuwajulia hali majeruhi akiwemo Dkt. Mwanjelwa.

Kwa upande wake, Dkt. Mwanjelwa, akiwa hospitalini hapo alimshukuru Mungu kwa kumnusuru na kuuliza kama dereva wake aliyejulikana kwa jina moja la Bw. Rajab na Katibu Muhtasi wake, Bi. Amina Mwampashi, kama wako hai lakini aliambiwa wapo Hospitali ya Rufaa mjini Mbeya.

Bw. Rajabu (dereva wa Dkt. Mwanjelwa), ambaye alikimbizwa katika  Hospitali ya Ifisi, ameumia vibaya kichwani na miguu yote miwili wakati Bi. Amina alifariki dunia baada ya kuteketea kwa moto akiwa ndani ya gari la mbunge.

Taarifa zinadai kuwa, kati ya watu waliokufa katika ajali hiyo yumo askari polisi wa Kituo Kidogo cha Mbalizi, aliyetajwa kwa jina la PC Samson.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Bw. Kandoro alisema amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa ambapo Serikali itaangalia njia na mikakati ya kukabiliana na ajari.

Alisema hadi jana jioni miili ya watu walifariki pamoja na majeruhi walikuwa hawajatambuliwa.

“Majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Ifisi na Rufaa mkoani Mbeya ambako pia maiti za watu waliokufa zimehifadhiwa huko kwa ajili ya utambuzi zaidi,” alisema.

Wakati huo huo, Mwandishi wetu Benedict Kaguo, anaripoti kutoka  Handeni kuwa, basi la Kampuni ya Dar Express, jana limeteketea moto ambapo abiria 48 waliokuwa wakisafiri na basi hilo kutoka Rombo mkoani Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam, wakinusurika kufa.

Katika ajali hiyo ya moto ambayo ilitokea Kijiji cha Segera, Barabara Kuu ya Chalinze-Segera, mkoani Tanga na hakuna abiria aliyefanikiwa kuokoa mzigo wake.

Mmoja wa wafanyabiashara wa machungwa Mjini Segera, Bw. Sonda Makinyala, alisema basi hilo lilianza kuungua moto sehemu ya mbele upande wa dereva na hakuna mizigo iliyotoka ambapo abiria walijiokoa kupitia madirishani.

“Abiria walilazimika kutokea madirishani ili kuokoa uhai wao, wananchi walijaribu kuuzima moto bila mafanikio kwa sababu hakukuwa na gari la zima moto,” alisema.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Constanine Massawe, alithibitisha kutokea tukio hilo na kulitaja basi hilo lenye namba za usajili T 369 ARH, aina ya Scania.

“Tukio limetokea saa 5:30 asubuhi katika eneo la Segera, wilayani Handeni, basi hili lilikuwa likiendeshwa na Bw. John Mwakihaba (41), mkazi wa Dar es Salaam.

“Abiria mmoja ambaye alifahamika kwa jina la Bi. Jackline Kisanga (21), alijeruhiwa eneo la kichwani baada ya kuruka nje kutoka kwenye basi,” alisema Kamanda Massawe.

Alisema abiria huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Magunga kwa ajili ya matibabu baada ya kuangukia kichwa wakati akijaribu kujiokoa katika ajali hiyo.

Kamanda Massawe alisema mizigo yote ya abiria wa basi hilo imeteketea kwa moto ambapo uchunguzi wa polisi unaendelea ambapo thamani ya mali zilizoteketea haijaweza kufahamika.


No comments:

Post a Comment