11 September 2012

Waumini msitafute umaarufu kanisani'


Na Stella Aron

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, ametaka waumini wa kanisa hilo kuacha kutafuta umaarufu ndani ya kanisa hilo badala yake wamtumikie Mungu ili wapate baraka zaidi.


Alisema wapo baadhi ya waumini ambao waanatumia kivuli cha kanisa ili jamii iweze kuwatambua kwa masilahi binafsi.

Askofu Malasusa aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika ibada ya uzinduzi wa Kanisa la Wazo Hill, ambalo ujenzi wake ulianza mwaka 2001 na kugharimu zaidi ya sh. milioni 820.

“Wapo baadhi ya waumini wanaopenda jamii iwafahamu kwa kutumia kivuli cha kanisa na wasipopata nafasi ya kutambulika huwa ni shida kwao,” alisema Askofu Malasusa.

Aliwashukuru waumini wa kanisa hilo kwa kutoa michango mbalimbali na kuhakikisha ujenzi huo unamalizika licha ya kujitokeza changamoto mbalimbali.

Aliongeza kuwa, amaamini kuwa kamati iliyokuwa kusimamia ujenzi huo ilikumbana na changamoto nyingi lakini kwa uwezo wa Mungu wameweza kufika mwisho wa safari ya ujenzi.

Machungaji wa Kanisa hilo, Manase Lema, alisema wazo la ujenzi huo liliibuka mwaka 1996 katika maandalizi ya sherehe ya Jubile ya kutimiza miaka 25 ya KKKT, Usharika wa Wazo Hill baada ya kuonekana kanisa lililopo ni dogo hivyo haliwatoshelezi waumini ambao walikuwa wakiongezeka kwa kasi kubwa.

Alisema ujenzi huo umetokana na sadaaka za waumini na michango ya marafiki mbalimbali ambapo hivi sasa, sh. milioni 500 zinaitajika kwa ajili ya ujenzi wa shule ya watoto wa Jumapili.

No comments:

Post a Comment