11 September 2012

Kesi ya Kibanda yakwama kusikilizwa


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imeshindwa kuanza kusikiliza kesi ya kuwashawishi askari na maofisa wa majeshi nchini kuacha kuitii Serikali kutokana na Hakimu anayeisikiliza kesi hiyo Bi. Waliyarwande Lema, kutokuwepo mahakamani.

Kesi hiyo inamkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Bw. Absalom Kibanda pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Arusha, Bw. Samson Mwigamba.

Mshtakiwa mwingine ni Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Bw. Theophil Makunga ambapo jana ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Frank Moshi aliihairisha kesi hiyo baada ya Hakimu Lema kupata udhuru hivyo itasikilizwa Oktoba 22 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, wakili wa Serikali Bw. Prosper Mwangamila aliiambia mahakama hiyo kuwa walikuwa na mashahidi wawili Bw. Raphael Okololo na Bw. George Mwampashi ambao walikuwa tayari kutoa ushahidi wao.

Desemba 2011 ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili (Mwigamba na Kibanda), wanakabiliwa na kosa la kuandika makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka maalum kwa askari wote”.

Ilidaiwa kuwa Bw. Mwigamba ambaye aliwahi kuwa Mhasibu wa CHADEMA, na Bw. Kibanda, wote kwa pamoja waliandika na kuiruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye Gazeti la Tanzania Daima, toleo namba 2552 la Novemba 30,2011.

Ilielezwa kuwa, makala hiyo ya uchochezi ilichapishwa na mshtakiwa wa tatu Bw. Makunga kupitia kiwanda cha uchapaji kilichopo chini ya uongozi wa Mwananchi Communication Ltd.

No comments:

Post a Comment