11 September 2012

TANPRESS yasikitika ukimya wa JK


Neema Kalaliche na Jane Hamalosi

SHIRIKA Huru la Habari nchini (TANPRESS), limesikitishwa na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, kushindwa kutuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha mwandishi wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw. Mobin Sarya, alisema Rais Kikwete amekuwa na kawaida ya kutuma salamu za rambirambi katika misiba lakini kwa marehemu Mwangosi ameshindwa kufanya hivyo.

“Mimi najiuliza Rais Kikwete na Dkt. Mukangara wanajiweka katika kundi gani, inasikitisha leo hii kiongozi wa nchi anaponyamazia maovu katika utawala wake.

“Japokuwa matamko mbalimbali yametolewa kulaani mauaji haya ambayo yamefanywa na polisi, viongozi wa Serikali na taasisi zake hawajalichukulia kwa uzito tukio hili ndio maana hadi sasa hakuna aliyekwenda kutoa pole kwa familia yake,” alisema.

Alisema TANPRESS wanatoa wito kwa Rais Kikwete awafukuze kazi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kushindwa kuwajibika kutokana na ukatili wa polisi wao na Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda, akamatwe kwa kutoa amri ya iliyosababisha vurugu na mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment