05 September 2012

Watendaji wapewa miezi mitatu warejeshe eneo


Na Peter Mwenda

MBUNGE wa Ukonga, Dar es Salaam, Bi. Eugen Mwaiposa, ametoa miezi mitatu kwa watendaji wa Serikali ngazi ya kata kurejesha eneo la Kituo cha Afya Pugu Kajiungeni, vingenevyo ataruhusu nguvu ya umma utumike.

Akizungumza juzi katika uzinduzi wa kituo hicho, Bi. Mwaiposa alisema eneo hilo linadaiwa kuvamiwa na mfanyabiashara aliyeweka mnara wa simu na nyumba ya kuishi wakati Serikali imelitenga kwa ajili ya huduma za jamii.

Alisema kituo hicho ambacho kimeanza kutoa huduma, kina wodi 14 ambazo zitatumika kulaza wagonjwa wa jinsi zote.

“Maeneo yaliyotengwa kwa huduma za jamii hayapaswi kuguswa, wanaovamia mali zao zitaharibiwa ambapo uvamizi huu unatokana na baadhi ya viongozi serikalini kutokuwa waaminifu badala yake wanaingia mikataba feki na wafanyabiashara.

“Mkiona eneo lenu la huduma za jamii limevamiwa, mfuateni kiongozi wanu, kama atashindwa kutoa majibu ya uhakika tumieni nguvu zenu kuzuia aina yoyote ya ujenzi,” alisema Bi. Mwaiposa.

Diwani wa Kata ya Pugu Kajiungeni, Bi. Imelda Samjela, alisema kituo hicho kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa ambazo hazitoshi kutosheleza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa.


“Tunaagiza dawa nyingi lakini tunapewa kidogo, kondomu tunapewa nyingi sana ambazo hadi sasa hazijaisha mbali ya kuagizwa muda mrefu,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya kituo hicho, Bw. Abdallah Kiranga, alisema changamoto iliyopo ni uhaba wa maji, wafanyakazi na ukosefu wa jenereta la kuwasha umeme.

“Tunahitaji kuwekewa uzio ili wavamizi wengine wasipate nafasi kutuingilia, pia tunaomba tupate chumba cha kufanyia upasuaji,” alisema Bw. Kiranga.

Aliongeza kuwa, kituo hicho kinatoa huduma ya matibabu kwa wakazi wa kata hiyo na zingine za jirani kama Majohe, Gongo la Mboto na Chanika ambao walikuwa wakienda Kisarawe.

Akijibu maombi hayo, Bi. Mwaiposa aliahidi kujenga kisima kirefu cha maji ndani ya kituo hicho, kufuatilia upatikanaji wa madaktari, dawa na jenereta.

No comments:

Post a Comment