05 September 2012

Ligi Kuu Zanzibar kuanza J'mosi



Na Mwandishi Wetu

LIGI Kuu ya Zanzibar 'Grand Malt Premier League', inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi ambapo Super Falcon watafungua pazia na Chipukizi, katika Uwanja wa Gombani, Pemba.


Siku hiyo pia kutakuwa na mechi nyingine ya ufunguzi ambapo KMKM itapepetana na Mafunzo katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) na kusainiwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Ali Mohamed ilieleza kwamba kila kitu kuhusiana na ligi hiyo kimekamilika .

Mohamed alisema, timu zote tayari zipo tayari kwa ajili ya ligi hiyo na amezitaka zifanye kila wawezalo kuhakikisha wanapata ushindi wa haki.

Kiongozi huyo alisema ligi hiyo itaendelea tena Jumapili kwa kuzikutanisha timu za Malindi na Bandari kwenye Uwanja wa Amaan, huku Duma na Jamhuri wakikutana Gombani.

Alisema Jumatatu itakuwa ni kati ya Mtende na Zimamoto, wakati siku inayofuata ni Chuoni na Mundu. Mechi zote hizo zitafanyika katika Uwanja wa Amaan.

Naye Waziri Asiye na Wizara Maalumu Zanzibar, Machano Othman Said, aliishukuru Grand Malt kwa kudhamini ligi hiyo na kusema italeta ushindani mkubwa.

"Huu ni mwanzo mzuri kwa soka la Zanzibar na naamini tutafikia mafanikio tuliyokusudia. Nawashukuru Grand Malt kwa udhamini huu.

"Ila ninawaomba wadau wote wa ligi hii kuanzia Grand Malt, ZFA na klabu kuweke wazi mikataba yote ili kusiwe na manung'uniko," alisema.

Naye Meneja Masoko wa Grand Malt, Fimbo Butallah alisema wamejipanga kuhakikisha ligi hiyo inakuwa bora zaidi.

Grand Malt kinywaji kisicho na kilevi imeingia mkataba wa kuidhamini ligi hiyo kwa muda wa miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment