05 September 2012

Wassira abanwa na wapiga kura jimboni


Na Raphael Okello, Bunda

AHADI alizotoa Mbunge wa Jimbo la Bunda, mkoani Mara, Bw. Stephen Wassira, kwa wapiga kura wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2005, zimemuweka mahali pabaya baada ya wananchi kutaka maelezo ya kina juu ya sababu zinazochangia ahadi hizo kutotekelezwa kwa wakati kama walivyotarajia.


Bw. Wassira ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Ueatibu, alikumbana na swali hilo juzi katika kitongoji cha Manyamanyama mjini hapa akiwa katika ziara ya kutembelea wapiga kura wake.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Bw. Mgendi Mukajanga, alitaka kujua sababu ya Serikali kuchelewesha mradi wa maji safi kama alivyoahidi katika kampeni zake.

Kutokana na swali hilo, Bw. Wassira aliwataka wananchi kuwa wavumilivu na kusisitiza kuwa, mchakato wa utekelezwaji mradi huo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia unaendelea vizuri.

“Kimsingi nimechoshwa na matusi yanayotokana na kuchelewa kwa mradi huu, mradi huu unaendelea vizuri sana jambo la msingi tuwe na subira wakati jitihada za kuufanikisha zikiendelea.

“Mradi huu ukikamilika nitalala usingizi…kama matusi yangekuwa yanaua, ningekuwa nimekufa, siwezi kuogopa kuja jimboni kwangu kwa sababu ya kuhojiwa masuala ya maji, nitaendelea kuja na kutoa majibu sahihi kuhusu hatua ambazo Serikali inazichukua,” alisema.

Alisema kama asipoenda jimboni, baadhi ya wanasiasa watakwenda kuzungumza mambo ya uongo ambao ndio mitaji yao na kuongeza kuwa, Tanzania ni kubwa na ina miradi mingi ambayo imekwama ukilinganisha na mradi huo.

Alitolea mfano wa mradi wa maji uliopo Mjini Mgumu, mkoani Mara ambao licha ya Bwawa la Manchira kujengwa na Serikali miaka saba iliyopita, wakazi wake hawajapata maji hadi leo.

Bw. Wassira alisema kutokana na ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Maji, alilazimika kutafuta wafadhili ambapo Benki ya Dunia nayo ilikubali kuufadhili mradi huo.

“Hadi sasa tangi la maji limejengwa katika Mlima Kaswaka, nyumba mbili za pampu ambazo zimejengwa eneo la Migungani na moja kwenye chanzo cha maji Nyabehu, kilichopo Ziwa Victoria.

Aliongezea kuwa, mitalo ya kutandaza mabomba kutoka chanzo cha maji Nyabehu kwenda mjini Bunda imeanza kuchimbwa pamoja na kujengwa  miundombinu ya umeme kutoka Nyantare kwenda nyumba ya kusukuma maji ambapo ujenzi wa chunjio nao  inatarajiwa kuanza karibuni.

Wananchi hao pia walitaka kujua hali ya huduma katika Hospitali Teule ya Wilaya hiyo (BDDH), ambayo huduma zake ni mbovu na kuiomba Serikali ione umuhimu wa kukipandisha hadhi Kituo cha cha Afya Manyamanyama, kiwe Hospitali ya Wilaya.

Walisema kutokana na uhaba wa maji mjini hapa, huduma za afya zimezidi kudorora katika Hospitali ya Wilaya ya Kituo cha Afya Manyamanyama ambapo wagonjwa kulazimika kuyanunua nje.

Kuhusu Kituo cha Afya Manyamanyama kupandishwa hadhi, Bw. Wassira alisema tayari amewasilisha hoja hiyo Wizara ya afya na Ustawi wa Jamii ambayo ipo katika mchakato wa kuvunja mkataba na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

“Hadi sasa kulingaana na mkataba uliopo, Serikali bado inagharamia huduma mbalimbali DDH hadi itakapovunja mkataba ili fedha hizo zihamishiwe Manyamanyama.

Alihadharisha kuwa kama Serikali itavunja mkataba huo, hospitali ya DDH haitafungwa bali gharama za tiba zitapanda zaidi ya sasa.

No comments:

Post a Comment