05 September 2012

Wananchi wavamia chanzo cha maji Nyakahanga


Na Livinus Feruzi,
Karagwe

CHANZO cha maji kwenye bonde la Nyakagera kinachotegemewa na Hospitali teule ya Wilaya ya Nyakahanga kwa ajili ya upatikanaji wa maji katika shughuli za kila siku, kiko hatarini kukauka baada ya wananchi kukivamia na kuanzisha makazi.


Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyakahanga wilayani Karagwe, Dkt. Andrew Cesari alisema chanzo hicho kinachomilikiwa na hospitali hiyo kinatishiwa usalama wa maji ikiwemo kukauka baada ya ujenzi wa nyumba karibu na chanzo hicho kujengwa kwa wingi.

Dkt. Cesari alisema licha ya hospitali hiyo kulipia ada kila mwaka kwa mamlaka ya bonde la Ziwa Victoria kwa ajili ya umiliki na gharama kubwa za uendeshaji wa
mitambo ya maji bado hospitali inakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji ya uhakika.

Alisema kila mwezi kati ya sh. 600,000 hadi 700,000 zinatolewa na hospitali hiyo kama gharama za kuendeshea mitambo ya kusukuma maji, lakini upatikanaji wa maji
kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa na hospitali kwa ujumla yamekuwa ya shida.

"Mheshimiwa mgeni rasmi hospitali inacho chanzo cha maji kwenye bonde Nyakagera lakini tatizo linalotukabili kwenye chanzo hiki kutishiwa usalama wa maji na pia kukauka kwani ujenzi wa nyumba za makazi karibu na chanzo hiki umeshika kasi kubwa," alisema.

Alisema mbali na kutishiwa kukauka kwa chanzo pia hospitali hiyo inakabiliwa na
uchakavu wa mitambo inayohitaji ukarabati wa mara kwa mara na unahitaji gharama kubwa.

"Suala la upatikanaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani ni tatizo kubwa kwa hapa Karagwe, hospitalini tumekuwa tukishuhudia madhara haya kwa kupokea wagonjwa wengi kutokana na kutumia maji yasiyo salama ikiwemo wengine kupoteza maisha," aliongeza mganga huyo.

Kutokana na hali hiyo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bw. Fabian Massawe na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kuhakikisha wanashughulikia tatizo la uvamizi wa wananchi ili kunusuru chanzo hicho na maisha ya wagonjwa.

Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya jubilee ya miaka 100 ya hospitali hiyo Profesa Tibaijuka alisema sheria za mazingira katika vyanzo vya maji ziko wazi na kuwa wananchi hawatakiwi kujenga kwenye vyanzo vya maji na kuongeza kuwa maji katika
hospitali ni kitu muhimu.






No comments:

Post a Comment