10 September 2012

Mpango kasi uwezeshaji wanawake kielelezo cha ukombozi kwao


Na Darlin Said   

MPANGO Kasi wa Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana ni kielelezo tosha cha ukombozi kwa ajili viongozi wanawake.


Pia ni mpango unaolenga kuwatetea Mama zetu, Mabinti zetu, tumaini letu ambalo mpaka sasa linakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kiuchumi,kisiasa na kijamii

Mpango huu umeanzishwa na Taasisi ya Manawake na Maendeleo (WAMA) baada ya kuona kwamba wanawake na wasichana  ni mkono unaoliinua Taifa, hivyo mkono uletao mwana ndio uleao Taifa.

Akizindua Mpango huo hivi karibuni Mama Salma Kikwete anasema ni moja ya juhudi za pamoja za kuboresha hadhi ya wanawake na wasichana nchini Tanzania ili kuleta mabadiliko makubwa kwa afya ya Watanzania na kusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA anasema ingawaje Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto, kutokana na sera nzuri pamoja na juhudi mbalimbali za serikali na wadau wote wa maendeleo, lakini bado changamoto ni nyingi,hivyo ni jukumu la kuzitafakari.

Changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake wanaofariki wakiwa na ujauzito au wakati wa kujifungua ama kwa kukosa huduma za afya kwa sababu ya miundombinu, elimu, mila na desturi potofu.

Naye Katibu Mtendaji wa WAMA Bw.Nasibu anasema Mpango huo  unajumuisha dhana ya kutoa elimu,kuzuia ukatili na kuboresha uzazi wa mpango baada ya kugundua wanawake walio wengi wanakabiliwa na changamoto.

Anasema kupitia kampeni watatoa elimu kwa wanawake na wasichana kuhusu athari za kuzaa utotoni,kuzaa ukiwa na umri mkubwa na kumuezesha kufahamu njia za uzazi wa mpango kama njia pekee ya kukabiliana na tatizo hilo ili kuweza kufanikisha kufikia malengo ya kimaendeleo katika jamii.

Kwa upande wa Mama Kikwete anasema tatizo la vifo vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika ni miongoni mwa matatizo ambayo wanawake wanakumbana nayo hasa wale waisho vijijini.

Anasema matatizo hayo yamedhihilika katika simulizi ya iliyojulikana kwa jina la siku, ambayo inagusa maisha halisi ya wanawake wa kitanzania na kuvuta hisia za watu.

Simulizi hiyo inamlenga Sikudhani aliyekuwa na ndoto za kuwa muuguzi lakini alikosa na kujikuta akiacha shule akiwa darasa la nne na kuolewa akiwa na umri mdogo wa miaka 17 na kuzaa watoto sita ambapo wawili walifariki kabla hawajatimiza miaka mitano.

Sababu zilizomfanaya aache masomo ni pale familia  yake lipomtaka afanye kazi ili achangie katika pato la familia.

Simulizi hiyo anafafanua "Siku hakuweza kushirikishwa katika kufanya maamuzi kwa madai kuwa alikuwa mdogo badala yake mambo yote yalifanywa na Musa ambaye alikuwa mume wake"alisema Mama Salma Kikwete alipokuwa akiielezea simulizi hiyo.

Wakati huo huo alidiriki kumpiga pale anapokosea
humpuuza,kumfokea na kumtishia maisha yake"hayo ndio yalikuwa maisha ya Siku na mume wake".alisema Mama Kikwete

"Musa huwa anatumia mabavu na kumnyanyasa hata akiunguza chakula"jamani maisha kama haya ni hatari kwa akina mama na wasichana, hakuna dini inayoruhusu udhalilishaji wa namna hii".Ananasisitiza Mama Kikwete

Anasema kutokana na hali hiyo Siku anavumilia ukatili huo kwa kuwa hajui la kufanya kwani  katika jamii anayoishi, ukatili wa nyumbani unachukuliwa kama suala binafsi ambalo halitakiwi kuzungumzwa nje ya familia hivyo analazimika kukaa kimya.

Mama Salma anaendelea kufafanua kuhusu simulizi ya Siku  na kusema wakati mwingine Siku hujiuliza maisha yake yangekuwaje iwapo angeendelea na masomo? Je kama angekuwa anashiriki kufanya maamuzi yanayohusu kupanga familia yake, ingekuwa hivi?

"Hadithi kama ya Siku si ngeni kwetu hivyo ilikuepusha hali hiyo isindelee lazima tuboreshe maisha ya wanawake na mabinti zetu kwa kuimarisha afya ya mama na mtoto, elimu ya kupanga uzazi kuzungumzia mila na desturi zinazoendeleza ukatili wa kijinsia"anasema

Anasema takwimu zinazonyesha katika kila vizazi 10, 6 huwa katika mazingira hatari kama kuzaa watoto katika umri  mdogo.

Anasema uzazi unakuwa wa hatari iwapo mwanamke atapata ujauzito katika umri mdogo ama mkubwa mno, hivyo  anayezaa umri mdogo anahatarisha maisha yake na ya mtoto kwa vile viungo vya mwili wake havijawa tayari kubeba ujauzito.

Ansema vifo vya wakina mama wanaofariki wakati wakujifungua kwa kiwango kikubwa huwa ni vya mama aliye na umri mdogo au mkubwa.

"Nchini Tanzania, mmoja kati ya watoto 20 hufa kabla hawajatimiza umri wa mwaka mmoja. moja kati ya watoto 12 hufa kabla hajatimiza umri wa miaka mitano,"anasema. 

Anasema hivyo kwa sasa katika kila vizazi hai 1,000 watoto wachanga 51 na walio chini ya miaka mitano 81 hufariki.

Kupanga uzazi kwa wanawake na wanaume kunasaidia kupunguza viwango vya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kwa zaidi ya asilimia 40.

"Hivyo wakati umefika kwa akina baba na akina mama ukakaa pamoja kujadiliana kivipi mtaweza kuzaa kwa mpangilio ili kuleta kizazi kilicho bora.

Anasema ukweli ni kwamba asilimia 70 ya wanawake hupenda kusubiri miaka miwili kabla ya kupata watoto wengine au huwa hawapendi kupata watoto wengine zaidi. Hata hivyo nchini Tanzania ni wanawake watatu tu kati ya 10 walioolewa ndio hutumia uzazi wa mpango.

Karibu nusu asilimia 46 ya mimba zote nchini mwetu huwa hazikutarajiwa,takwimu hizo zimepetikana kupitia muongozo wa Sera ya Taifa 2011.

Anasema ingawaje utumiaji wa uzazi wa mpango kwa wanawake walioolewa umeongezeka kwa asilimia 18 toka mwaka 2004-hadi 2005 asilimia 24 mwaka 2010, lakini  bado vipo vikwazo katika utumiaji wa njia za uzazi wa mpango.

"Vikwazo hivyo ni pamoja na ukatili wa kijinsia,baadhi ya  mila na desturi,ukosefu wa uelewa na maarifa na ugumu wa kupata huduma sahihi, ushirikishwaji wa jamii hasusani wanaume, pamoja na  fikra potofu,"anasema.

Anasema Tanzania imefikia usawa wa kijinsia katika kujiunga na elimu ya msingi, idadi ya watoto wa kike na kiume karibia inalingana na karibu asilimia 95 ya wavulana na wasichana wanaandikishwa.

"Historia inaonyesha kuwa , wasichana wachache uhudhuria na kumaliza elimu ya sekondari. Huko vijijini asilimia ya wasichana waliojiunga na shule za sekondari ni ndogo zaidi, na zipo tofauti kubwa kati ya mkoa na mkoa.

Asilimia 29.9 tu ya wasichana wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 wanasoma katika shule za sekondari,"anasema Mama Salma.

Aidha kwa upande wa kiwango cha ukatili dhidi ya wasichana. Vijana wa kike watatu kati ya wanne (asilimia 74) walio chini ya umri wa miaka 18 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili na ndugu, mtu mwenye madaraka au mwenzi wake.

Takribani asilimia 6 ya wanawake na wasichana wamewahi kulazimishwa kufanya tendo la ngono kabla hawajafikia umri wa miaka 18. kwa mujibu wa UNICEF. 


"Utetezi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake una  changamoto kubwa, kwa sababu   wanaume na wanawake wengi na jamii kwa ujumla wanaamini kwamba ukatili huo unavumilika,"anasema Mama Salma.

Anasema Tanzania  wanaamini kwamba kupigwa na mume ni jambo linalokubalika. hii ina maana kwamba ni wakati wa kubadili mitazamo juu ya matendo ya ukatili kwa wanawake na wasichana ndani ya jamii kwa kulizungumzia jambo hili waziwazi.

Utafiti unaonyesha kwamba kadiri wanawake wanavyoshiriki katika uamuzi wa mambo ya kifamilia ndivyo wanavyoweza kuamua mustakabali wa afya yao ikiwa ni pamoja na malengo yao ya uzazi.

Asilimia 27 ya wanawake ambao hawashiriki uamuzi wa masuala ya kifamilia hutumia uzazi wa mpango, ambapo asilimia 40 ya wanawake wanaoshiriki katika maamuzi ya nyumbani wanatumia uzazi wa mpango.  

Kupitia Mpango Kasi wa  uwezeshaji Wanawake na Wasichana unatarajiwa kutekelezwa nchini Tanzania baada ya kujaribiwa katika nchi nyingine ili kubaini matokeo ya ongezeko la idadi ya watu kwa jamii na malengo ya maendeleo.

Anasema upimaji na ufuatiliaji wa utekelezaji na matokeo ya  mpango huo utafanyika kisayansi kwa kutumia teknolojia  ya kisasa kwa kutumia programu maalum ya komputya.

Anasema msingi wa mpango huo ni uwekezaji katika mikakati ya kuboresha Afya ya mama na mtoto, elimu na kupiga vita mila na desturi zinazosababisha ukatili dhidi ya wanawake.

Katika Mpango huu  utahakiakisha unawawezesha wasichana kuendelea na elimu ya msingi hadi chuo kikuu kwa kuweka vipaumbele katika  upatikanaji wa nyenzo  kwa ajili ya elimu na huduma za uzazi wa mpango.

Anasema mbali na hilo utamahasisha upatikanaji wa nyenzo kwa ajili ya utekelezaji wa Sera, Miongozo na Mikakati ya taifa  ya kuzuia ukatili wa kijinsia.

Anasema tatizo la kijinsia linapelekea kuwepo kwa matatizo ya kiafya kwa wanawake ikiwemo mauaji ya wanawake, mimba zisizo tarajiwa vifo vitokanavyo na uzazi magonjwa ya pamoja na usongo wa mawazo na wasiwasi,"anasema.


No comments:

Post a Comment