Na Mariam Mziwanda
SERIKALI imejadili mikakati ambayo itasaidia uwepo wa Sera ya Taifa ambayo itatumika kusimamia mashirika ya umma ili yaweze kuhudumia wananchi badala ya kusababisha hasara serikalini.
Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kongamano ambalo lilijadili mfumo bora wa kuendesha Mashirika ya Umma nchini.
Alisema kuyaondoa mashirika hayo katika utegemezi wa ruzuku, lazima kuwapo na sera madhubuti ambayo itasimamia uendeshaji wake.
“Kwa sababu ya ukosefu wa Sera ya Taifa inayodhibiti mianya ya rushwa na matumzii hewa, ndio chanzo cha mashirika haya kutokuhudumia wananchi ipasavyo na kuwa tegemezi.
“Mashirika yetu hayazingatii ushindani hivyo ipo haja ya kuwapo sera itakayowafanya wajumbe wa bodi, utawala na watendaji kuwa wawajibikaji kisheria, waaminifu, wenye kuheshimu utawala na kulijengea Taifa uwezo,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema upo umuhimu mkubwa wa kuwepo sera ambazo zitasimamia mashirika hayo.
“Mashirika yetu yamejaa rushwa, hata wasimamizi wake wakuu hawafuati misingi ya utawala bora pamoja na wanasiasa kuingilia kati maamuzi ya mashirika kwa faida zao binafsi hivyo kwa msingi huu nchi ipo mikono mwa wanasiasa,” alisema.
Bw. Kabwe alisema mashirika hayo ndio kichocheo cha upotevu wa mapato ya nchi hivyo ipo haja kuwepo sera na kipengele ambacho kitawaondoa wabunge kushiriki ujumbe wa bodi ili kuyajengea uwezo na kuondoa utetezi wa utendaji mbovu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kongamano Balozi Juma Mwapachu, alisema uratibu bora wa sera kwa mashirika hayo itaondoa muingiliano wa kazi zake.
No comments:
Post a Comment