24 September 2012

KKKT kuwaombea madiwani Moshi


Na Gift Mongi, Moshi

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mwangaria Kahe, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, umejipanga kuwaombea madiwani wa manispaa hiyo ili waondokane na pepo mchafu anayewatuma kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Akizungumza na gazeti hili, Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, Richard Njau, alisema kitendo cha madiwani hao kutaka kutumia sh. milioni 200 kwa ziara ya kimafunzo Kigali nchini Rwanda ni jambo lisilowezekana hivyo wanastahili kuombewa.

“Sioni haja ya madiwani hawa kwenda kujifunza suala la usafi wa mazingira nchini Rwanda, mji wetu ni msafi sana hivyo safari yao haikuwa na tija zaidi ya kufuja fedha,” alisema.

Aliongeza kuwa, fedha walizotaka kutumia kwa safari hiyo ni kodi ya wananchi ambayo walipaswa kuitumia vizuri kwa kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kuishia mikononi mwa wachache.

Alisema kama utekelezaji wa miradi ya maendeleo umekamilika, fedha hizo ni vyema zikatumika kwa kuratibu mahubiri ya neno la Mungu ili watu walipotea waweze kuzingatia mafundisho yake.

Mchungaji Njau alisema mara nyingi kanisa limekuwa likikemea wizi na ufisadi lakini wanaosikia ni wachache kuliko wasiosikia hivyo aliwasihi madiwani kuwa wasikivu.


No comments:

Post a Comment