24 September 2012

CHADEMA waanza kumkwepa Tendwa


Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeanza kukacha ushirikiano wake na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini , Bw. John Tendwa baada ya kukataa mwaliko wa kushiriki semina inayofanyika leo wakisubiri hatua atakazochukua Rais Jakaya Kikwete kuhusu mauaji ya kisiasa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, imesema chama hicho kimefikia uamuzi huo kwa kile walichodai utendaji dhaifu wa kipropaganda unaooneshwa na Bw. Tendwa.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, alisema utendaji huo umesababisha Kamati Kuu ya chama hicho kujiridhisha kuwa adui wa demokrasia na hafai kuendelea kuwepo katika nafasi aliyonayo.

“Kamati Kuu iliazimia kuwa, pamoja na kuendelea kuheshimu sheria ya vyama vya siasa, CHADEMA haitashiriki shughuli zozote ambazo zitasimamiwa na Bw. Tendwa, hadi atakapoondolewa kwenye nafasi yake na kuteuliwa msajili mwingine.

“Ikumbukwe kuwa, tulifanya kikao maalumu kilichojadili hali ya siasa nchini kutokana na mfululizo wa mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi katika shughuli za kisiasa za CHADEMA,” alisema.

Alisema pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu iliazimia kumuandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumtaka achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.

Bw. Mnyika alisisitiza kuwa, CHADEMA hakitashiriki semina inayofanyika leo.

No comments:

Post a Comment