11 September 2012

Waislamu wasisitiza kuvamia BAKWATA


Stella Aron na Rehema Maigala

WAUMINI wa dini ya Kiislamu jijini Dar es Salaam, wameazimia kufanya mkutano wa pamoja ambao utashirikisha Waislamu kutoka mikoa yote nchini ili kwenda kuvamia Ofisi za Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA), kushinikiza viongozi kuondoka madarakani.


Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Katibu wa Jumuiya na Tasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, alisema Waislamu hawawezi kuwavumilia viongozi ambao wamewageuka na kuanza kuuza mali za Waislamu.

“Hatuwezi kuwavumilia viongozi wa namna hii ndio maana tunafanya maandamano ambayo yatashirikisha Waislamu wote kutoka mikoa mbalimbali tukimaliza mkutano wetu,” alisema.

Shekhe Ponda aliongeza kuwa, hatua ya viongozi wa BAKWATA kuuza rasirimali za Waislamu si jambo la kufumbiwa macho hivyo wamechoka na tabia hiyo na sasa wanadai haki zao.

Alisema watahakikisha wanafanya mageuzi ya ufisadi ndani ya BAKWATA ili kupata viongozi wanaotii sheria si kuwageuka.

“Kituo cha Elimu cha Markazi kilichopo Changombe, kimeuzwa hii ni hatari kama tukiendelea kufumbia macho uuzwaji mali za Waislamu, wachache ndio wanaonufaika,” alisema.

Akizungumzia makubaliano yaliyofikiwa Ijumaa kati yao na Serikali, Shekhe Ponda alisema tayari yameanza kuzaa matunda baada ya Waislamu waliokuwa wakishikiliwa katika Vituo vya Polisi kuachiwa kwa dhamana.

Alisema leo wanatarajia kukutana ili kujadili suala la baadhi ya Waislamu waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo ili kesi zao ziweze kufutwa na kuachiwa huru.

Mwenyekiti wa Mihadhara, Shekhe Kondo Bungo, ameiomba Wizara wa Mambo ya Ndani ya Nchi, iwachie huru Waislamu wote waliokamatwa kwa tuhuma za kutoshiriki au kuhamasisha watu wasishiriki Sensa ya Watu na Makazi ili kuheshimu makubaliano.

Wakati huo huo, kutokana na hofu ya Waislamu kuvamia ofisi za BAKWATA, jana askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walizingira ofisi hizo wakiwa na silaha pamoja na maji ya kuwasha ili kukabiliana na uvamizi huo.

No comments:

Post a Comment