11 September 2012
Rufaa ya Mpendazoe sasa yatupwa
Na Rehema Mohamed
HATIMAYE Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman, ameiamuru Mahakama ya Rufaa nchini kuondoa mahakani hapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa ya kupinga ushindi wa Mbunge Jimbo la Segerea, Dkt. Makongoro Mahanga (CCM).
Kusudio hilo liliwasilishwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Fred Mpendazoe.
Jaji Othman alitoa amri hiyo Agosti 2 mwaka huu, baada Bw. Mpendazoe, kuamua kuachana na dhamira yake ya kukata rufaa hukumu iliyotolewa awali.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Othman aliamuru taarifa hiyo iendolewe mahakamani hapo chini ya Kanuni ya 89 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009.
Taarifa ya Bw. Mpendazoe, kuachana na azma ya kukata rufaa iliwasilishwa mahakamani hapo Julai 12 mwaka huu, kupitia wakili wake, Bw. Peter Kibatala ambaye ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Awali Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu ya kesi hiyo Mei 2 mwaka huu, lakini Bw. Mpendazoe aliwasilisha Mahakama ya Rufaa taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Bw. Mpendazoe kupitia wakili wake, Bw. Kibatala aliwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo Mei 7 mwaka huu.
Katika kesi ya msingi aliyoifungua Novemba 10, 2010, Bw. Mpendazoe alikuwa akipinga ushindi wa Dkt. Mahanga akidai haukuwa huru kwani taratibu na Kanuni za Sheria ya Uchaguzi zilikiukwa katika kuhesabu kura, kujumlisha, kutangaza matokeo.
Aliiomba Mahakama itengue matokeo hayo na kuamuru uchaguzi mdogo uitishwe katika jimbo hilo au imtangaze yeye kuwa mshindi.
Walalamikiwa katika kesi hiyo walikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi (ARO) wa majimbo yaliyoko katika manispaa hiyo likiwemo Segerea na Dkt. Mahanga.
Dk. Mahanga alikuwa akitetewa na mawakili Bw. Jerome Msemwa, na Bw. Aliko Mwamanenge, AG na ARO walitetewa na Mawakili Waandamizi wa Serikali Bw. David Kakwaya na Bw. Seth Mkemwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment