11 September 2012
Membe akusanya ushahidi mgogoro wa Ziwa Nyasa
Na Cresensia Kapinga, Songea
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw.
Bernard Membe, amesema wananchi waishio mwambao wa Ziwa Nyasa, wasiwe na wasiwasi juu ya usalama wao kutokana na mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Tanzania na Malawi.
Alisema Taanzania itahakikisha wanalilinda, kulitetea na kulihifadhi ziwa hilo ambalo ni hazina kubwa wakazi wa Ruvuma na Taifa.
Bw. Membe aliyasema hayo mjini Songea, mkoani Ruvuma jana wakati akizungumza na wazee wa vijiji vya Mbambabay, Liuli na Lituhi kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya siku moja.
“Lengo la ziara yangu ni kutaka kuzungumza na wazee ambao ndio wanafahamu ukweli wa ziwa hili, leo (jana), nimekuja kwa shabaha mbili kwanza kuliona ziwa lenyewe na wale wanaolitumia uchumi wao ukoje pamoja na kero zao.
“Shabaha ya pili kuwahakikishia usalama wenu na mali zenu kwani tutahakikisha mgogoro kila utakapopelekwa tunashinda,” alisema.
Akizungumza na wazee wa Kijiji cha Mbambabay, Bw. Membe alisema yeye pamoja na wataalam wake wamekaa na kuangalia tatizo lililopo na kubaini ni dogo lakini wenzao wa Malawi hawaelewi na kuamua kulipeleka Mahakama ya kimataifa.
Akielezea ukweli wa ziwa hilo, mzee aliyefahamika kwa jina la Bw. Gideon Ndembeka(84), alisema kwa ufahamu wake kutokana na maelezo ya wazee wake, ziwa hilo ni mali ya nchi tatu ambazo ni Msumbiji, Tanzania na Malawi na mikapa yake ipo katikati ya ziwa.
“Kwa ufahamu wangu na maelezo ya wazee wangu Mbeya na Songea ni miji iliyopo Tanganyika, vitabu viwili vya History of Unversitis Mission to Church Afrika, vitawasaidia kutatua mgogoro huu na kujua mipaka ya ziwa hili iko wapi,” alisema.
Aliongeza kuwa, Malawi ni wakorofi kwa sababu ukweli wa mipaka ya ziwa hilo unafahamika hata meli zinazofanya safari kwenye ziwa zikifika katika mipaka ya nchi husika bendera ubadilishwa na kupandishwa nyingine kama ni Tanzania au Malawi.
Naye Mzee Daudi Filbet (82), mkazi wa Kijiji cha Liuli wilayani
Nyasa, alisema tangu tangu enzi za mababu zao, mpaka wa ziwa hilo upo katikati na kipindi hicho kodi walilipa kwa Wajerumani ambao ndio walikuwa watawala.
“Malawi haijatawaliwa na Mjerumani, Serikali inamchelewesha Raisi wao Mama Joyce Banda ni vyema wakamtandika, sisi kama wazee tuko tayari kumwaga damu kwa kupigania nchi yetu na hatupo tayari kudhurumiwa haki yetu,” alisema.
Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mbunda (74), alisema ziwa hilo halikuchimbwa bali limeumbwa na Mungu sasa iweje leo mwanamke mwenzao Ziwa Nyasa ni lao.
“Naiomba Serikali ichukue hatua za kisheria haraka ikiwezekana tupigane vita kwani tatizo hilo halikuanzia kwa Rais Banda bali hata enzi ya Rais Kamuzu Banda alianza ukorofi kama huu lakini serikali ilipojipanga kutaka kumwajibisha alibadili msimamo,” alisema.
Bw. Membe aliwapongeza wazee hao kwa kujua ukweli wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ambapo yeye atarahisisha kazi yake baada ya kwenda katika Mahakama ya Kimataifa kutokana na ushahidi uliopo na atawahitaji ili kutoa ushahidi wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment