11 September 2012

Kitenge, khanga kuwa vazi la Taifa



Na Amina Athumani

KITENGE na khanga vimeteuliwa rasmi kuwa vazi la Taifa, ambalo litaanza kuvaliwa katika sherehe za miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania zitakazoadhimishwa  Desemba 9, mwaka huu.


Khanga na kitengo vitakuwa katika sura inayotambulisha utamaduni wa Tanzania, ambapo baadhi ya alama zitakazoshamiri kwenye vazi hilo ni bendera ya taifa, wanyama, ngoma, mwenge wa uhuru,  ngao, ala za muziki wa asili, Mlima Kilimanjaro, madini na mazao.

Uteuzi huo umefikiwa na kamati iliyoundwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mwishoni mwa mwaka jana kwa nia ya kuchagua kitambaa ambacho kitakuwa vazi la taifa kwa kila Mtanzania kulitambua.

Akizungumza Dar es  Salaam jana wakati wa kuwasilisha ripoti inayoonesha michoro ya vazi hilo litakalokuwa katika mtindo wa khanga na kitenge, Katibu wa kamati hiyo, Angel Ngowi alisema kazi ya kusaka kitambaa cha vazi la taifa lilianza tangu mwaka 2003.

Alisema mchakato huo uliwashirikisha Watanzania kwa kutoa maoni yao juu ya muonekano wa vazi hilo.

Ngowi alisema ili kufikia malengo hayo waliandaa mashindano ya michoro yaliyoshirikisha wasanii 88, ambao waliwasilisha michoro 200.

Alisema kati ya wasanii hao, sita ndiyo waliotimiza vigezo na matakwa ya vazi la taifa, ambapo wasanii hao waliunganishwa na wataalamu wa vitambaa kwa ajili ya kutengeneza jinsi vazi hilo litakavyoonekano katika khanga na kitenge.

Katibu huyo alisema wataalamu pamoja na wasanii hao walitengeneza michoro mitano yenye muonekano tofauti, katika kitenge na michoro minne yenye muonekano tofauti kwenye khanga ambayo ndiyo iliyowasilishwa jana kwa Waziri Fenella Mukangara.

Kutokana na kazi hiyo kukamilika, Waziri Fenella ameishukuru kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Joseph Kusaga.

Waziri Fenella ameiagiza Wizara yake chini ya Usimamizi wa Katibu Mkuu, ichague michoro minne kati ya iliyowasilishwa na kamati hiyo, ili ipelekwe Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na Kamati ya Ufundi ya Makatibu Wakuu kuipitia.

Alisema mchakato huo anategemea utafikia tamati Oktoba 31, mwaka huu  ili viwanda vya nguo vihamasishwe  kuzalisha kwa wingi na kwa ubora kwa Khanga na vitenge  vilivyoteuliwa.

Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Mustapha Hasanali, Ndesumbuka Merinyo, Joyce Mhavile, Angel Ngowi pamoja na wajumbe wengine.

No comments:

Post a Comment