12 September 2012

Waandishi watikisa nchi, Nchimbi mm! *Alazimishwa kuondoka mkutano wa wanahabari *Mikoani nako hapatoshi, wengine wazuiliwa



Na Waandishi Wetu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, jana amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuumbuliwa kwa kutimuliwa na waandishi wa habari baada ya kujitokeza kupokea maandamano yao yaliyolenga kulaani mauaji ya mwandishi wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daidi Mwangosi.

Marehemu Mwangosi aliuawa Septemba 2 mwaka huu, kwenye Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, akiwa kazini kwa madai ya kupigwa bomu na polisi waliokuwa wakipambana na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Tukio hilo la kuumbuliwa Dkt. Nchimbi, lilitokea jana katika Viwanja vya Jangwani, baada ya wanahabari hao kuhitimisha maandamano yao na kumkuta Waziri huyo eneo hilo kwa kile alichoeleza alitaka kusikiliza risala ya waandishi.

Kabla ya kutimuliwa, Dkt. Nchimbi alizomewa huku akionekana wazi kukosa amani ambapo wanahabari walisisitiza kuwa, Waziri huyo hawakumualika na jambo lolote ambalo angelizungumza, lisingeweza kukata kiu ya majonzi yao.

Wakati taratibu za kuanza kutoa matamko ya wanahari zinataka kuanza, Dkt. Nchimbi alipanda kwenye kifusi kilichotumika kutoa matamko yao jambo ambalo liliwashangaza wanahabari na kuanza kuhoji nani kamualika katika viwanja hivyo.

Kutokana na sintofahamu ya waandamanaji, zilianza kelele za kumtaka Dkt. Nchimbi aondoke eneo hilo na hata zilipopigwa kura za kuamua kama aendelee kubaki, waandishi walikataa asiendelee kuwepo kwa kunyoosha mikono na kupiga kelele.

“Aondoke...aondoke...atumtaki”, ndivyo walivyosema wanahabari wakimuangalia Dkt. Nchimbi usoni na kumpa waakati mgumu hivyo aliamua kuondoka akisindikizwa na sauti za waandishi wakisema; “puu...puu...puu” kuashiria mlipuko wa bomu na wengine wakisema msiba unawahusu waandishi wa habari.

Dkt. Nchimbi aliondoka eneo hilo akisindikizwa na Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Bw. Neville Meena, ambaye alimwambia “Tunakupenda, tunakuheshimu na tupo pamoja nawe”.

Maandamano ya kihistoria kulaani mauaji hayo yalianza saa tatu asubuhi katika Ofisi za Kituo cha Channel Ten, ambacho marehemu alikuwa akikifanyia kazi yakiongozwa na Wahariri.

Waandamaji walibeba picha ya marehemu Mwangosi na mabango yenye ujumbe mbalimbali na kusoimeka; “IGP Mwema hatuna imani na wewe kama vipi achia ngazi”.

Mengine yalisema; “Tunaomba kuwepo tume huru ya uchunguzi wa mauaji ya Daudi Mwangosi, Kamuhanda apelekwe The Hegue, Polisi wamemuua Mwangosi, Polisi ni chuna ngozi”.

Akizungumza baada ya kuyapokea maandamano hayo, Bw. Meena, alisema ni ishara tosha kuwa waandishi wameguswa na tukio hilo.

“Maandamano haya ni ya kihistoria kwani kitendo cha mwandishi wa habari kuuawa kikatili akiwa kazini tena mikononi mwa Jeshi la polisi ni cha kusikitisha,” alisema.

Alisema vyombo vya habari vina madaraka makubwa kuliko Jeshi la Polisi hivyo wakiamua kutumia kalama zao, hakuna anayeweza kuwakwamisha.

Aliongeza kuwa, wameamua kufanya maandamano hayo ili kufikisha ujumbe wao, badala ya kutumia kalamu na kamera zao kupambana na polisi.

Bw. Meena alisema kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari hata, Rais Jakaya Kikwete akitaka kuzungumza na Watanzania milioni 40 amekuwa akivitumia kufikisha ujumbe wake.

“Tumetokea mahala ambapo waandishi wa habari walikuwa wakipigwa, kujeruhiwa na sasa wanauawa jambo ambalo hatukubaliani nalo,” alisema Bw. Meena.

Alisema hatua ya maandamano ni ya pili ambayo ya kwanza ni kutoa matamko mbalimbali ya kulaani mauaji  ambapo ya tatu itafuatia baada ya tume iliyoundwa kumaliza kazi yake.

Aliongeza kuwa, hakuna mtu wala mamlaka yoyote ambayo itazuia vyombo vya habari kushindwa kufanya kazi yake kama vitafuata sheria, taratibu na kanuni.


Mwanachama wa TEF, Bw. Jose Kwayu, alisema mauaji aliyofanyiwa Mwangosi ndio mwanzo wa kubadilisha mwenendo wa Jeshi la Polisi.

“Watu wanalipa kodi kwa ajili ya kununua sare za polisi, viatu na vifaa vingine si kwa ajili ya kutumika kuulia walipa kodi,” alisema ambapo wanahabari walioshiriki maandamano hayo walisema, umefika wakati wa kuacha kuandika habari za polisi hadi tume iliyoundwa itakapomaliza kazi yake.

KILIMANJARO

Waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro, jana waliungana na wenzao kufanya maandamano ya amani ili kulaani mauaji ya mwenzao aliyeuawa kikatili akiwa kazini.

Katika maandamano hayo, waandishi walikuwa na mabango yaliyobeba ujumbe mbalimbali unaosema “Baada ya Mwangosi, polisi tuambieni nani anafuata ili tukitoka majumbani tuandike wosia kwa familia zetu”.

Mabango mengine yalisema; “Rais Kikwete ni mtaalamu wa kuomboleza misiba ya watu kama alivyofanya kwa marehemu Steven Kanumba (msanii wa filamu), lakini si kwa Mwangosi”.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani hapa (MECKI), Bw. Rodrick Makundi, alilaani mauaji hayo ambayo yameigusa jamii kubwa ya Watanzania.

“Ufike wakati polisi wawe na akili ya kujifunza kutokana na makosa badala ya kuendelea kumwaga damu za Watanzania wasio na hatia na nguvu kazi ya Taifa,” alisema.

MWANZA

Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Mwanza (MPC), nacho hakikuwa nyuma kuungana na wanahabari wenzao nchi nzima kufanya maandamano ya amani kupinga mauaji hayo.

Mbali ya kufanya maandamano, MPC kimetoa tamko la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchini pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema.

Chama hicho pia kimemtaka Rais Kikwete kumwajibisha Kamanda wa Polisi mkoani Iringa Michael Kamuhanda ambapo tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa MPC, Bw. Deus Bugaywa.

Maandamano hayo yalianzia katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya  Nyamagana, kupitia barabara za Nyerere, Lumbumba, Kenyatta, Posta na kuhitimishwa katika Uwanja wa Nyamagana wakiwa wamefunga midomo yao kwa plasta.

Waandishi walifanya maandamano hayo kwa lazima baada ya Jeshi la Polisi jijini hapa kuyazuia kwa madai kuwa, idadi ya askari polisi ambao wangewapa ulinzi haitoshi ambapo wengi wao wamepangiwa katika ziara ya Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda.

Bw. Bugaywa alisema MPC kimesikitishwa na mauaji ya mwanahabari mwenzao aliyeuawa na polisi akiwa kazini.

“Mauaji haya yamebadili sura ya Tanzania kimataifa kutoka kisiwa cha amani na kuwa cha mauaji, kabla marehemu Mwangosi hajafikwa na mauti, polisi walimzingira na kumpiga.

“Pamoja na kuwasihi wasimuue, hakusikilizwa badala yake wakamuua kwa kumpiga bomu, sisi tunajiuliza, kwanini polisi wageuke kuwa wauaji, nani kawatuma,” alisema.

Alisema kutokana na uzito wa mauaji hayo, pamoja na polisi kuzuia maandamano hayo hawakuwa tayari kuridhia agizo hilo kwani jeshi hilo halikuwa na mamlaka ya kuyazuia na yalikuwa ya amani.

BUKOBA

Mtikisiko wa maandamano hayo pia ulifanyika mkoani Kagera ambapo waandishi waliandamana kupinga mauaji hayo.

Maandano hayo yalianzia Kituo cha Mabasi mjini hapa kupitia Barabara za Jamhuri, Tupendane, Kagera Studio, Samuel, Luangisa, Uganda na kuishia Ofisi ya Chama cha Waandishi wa Habari mkoani hapa (KPC), yakiwa yamepewa ulinzi wa polisi.

Akizungumza baada ya kuyapokea,  Mwenyekiti wa KPC, Bw. John Rwekanika, alisema Serikali inapaswa kuwachukulia hatua za kisheria askari wote waliohusika na mauaji hayo.

Alisema kutokana na ushahidi wa picha, marehemu Mwangosi aliuawa kikatili jambo ambalo ni fedheha kwa Taifa linalohubiri amani, utulivu na utawala bora kwa kukiuka haki za binadamu.

“Katika eneo la tukio, alikuwepo Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda lakini alishindwa kumuokoa Mwangosi hivyo ni wazi kuwa ameshindwa kazi, awajibishwe,” alisema.


Katika maandamano hayo, waandishi hao walibeba mabango yenye ujumbe unaosema; “Tunaliangalia Jeshi la Polisi kama rafiki wa mashaka, mauaji ya Mwangosi na raia wengine ni kipimo cha kuzima uhuru wa habari na demokrasia”.

SINGIDA

Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya mkoani Singida (SINGPRESS), nao walifanya maandamano ya amani yaliyoanzia katika Banki ya NBC, kupitia Barabara za Kawawa, Lumumba, Msikiti, Ipembe, Karume, Kinyeto na kuishia ofisi za klabu hiyo.

Waandishi walibeba mabango yenye ujumbe tofauti unaolaani mauaji ya mwenzao ambapo Mwenyekiti wa SINGPRESS, Bw. Seif Takaza, aliyapokea na kusema kuwa, mauaji hayo yanatia shaka juu ya ukaribu uliopo kati wanahabari na Jeshi la Polisi.

MUSOMA

Jeshi la Polisi Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, jana liliwanyima waandishi kibali cha kufanya maandamano ili kuungana na wenzao kulaani mauaji hayo kwa maandamano ya amani.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Emmanuel Bwimbo, kitendo cha polisi kuwanyima kibali kimewanyima haki yao ya msingi kwani maandamano hayo yalipangwa kufanyika nchi nzima.

“Waandishi nchi nzima tulipanga kuandamana leo (jana), kwa amani lakini polisi walituzuia na sisi bado tunasisitiza kuwa, hatutaki mahusiano yoyote kati yao na sisi,” alisema.

SHINYANGA

Kama ilivyowatokea kwa waandishi wa haabari mkoani Mara, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga nalo lilizuia maandamano ya amani yaliyopangwa kufanywa na waandishi mkoani hapa.

Madai yaliyotolewa na jeshi hilo ni kuchelewa kwa barua ya kutoa taarifa ambayo haikuzingatia muda wa kuwasilishwa polisi.

Pamoja na juhudi za viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani hapa kukaa pamoja na Kamanda wa Polisi, Evarest Mangalla, bado aligoma na kushauri waandamane leo.

Kutokana na zuio hilo, waandishi wa habari mkoani hapa waliamua kuandamana kwa mtindo wa aina yake wakiwa wamebeba mabango yanayolaani mauaji ya mwenzao kwa kukaa nje ya barabara zilizopo kwenye ofisi za klabu yao na kufikisha ujumbe kwa wapita njia.

Mbali ya kufanya maandamano ya aina hiyo, chama hicho kilitoa tamko la kulaani mauaji hayo na kitendo cha polisi kuwazuia wasiandamane kwa hoja ambayo haikuwa na mashiko.

“Tunatangaza kuanzia leo tunasitisha rasmi kuandika habari za polisi na kufanya nao kazi hadi tofauti kati yetu na wao zitakapomalizika,” alisema Mwenyekiti wa klabu hiyo mkoani hapa, Bw. Shija Felician.

Waandishi wa haabari hii ni Gift Mongi, Suleiman Abeid, Veronica Modest, DamianoMkumbo, Theonestina Juma, Jovin Mihambi, Daud Magesa, Salim Nyomolelo na Goodluck Hongo.

1 comment:

  1. Kusema ukweli Nchimbi hana aibu kabisa,mbona hata kwenye mazishi ya mwandishi huyo aliyeuawa hatukumwona.Sijui kama alitoa hata salamu za rambirambi.Sasa anakuja kupokea maandamano?

    ReplyDelete