11 September 2012

Usafiri wa treni Dar kumaliza foleni



Na Mariam Mziwanda

USAFIRI wa abiria kwa njia ya treni jijini Dar es Salaam, umeanza jana kwa majaribio baada ya maandalizi ya awali kukamilika ambapo wakazi wa jiji hilo wameonekana kuufurahia.

Akizungumza baada ya kupanda usafiri huo kutoka Posta hadi Ubungo, Naibu Waziri wa Uchukuzi Bw. Charles Tizeba, alisema lengo la kuondoa tatizo la msongamano wa magari mjini.

Alisema ili kuhakikisha ahadi za Serikali kwa wananchi wake zinatekelezeka, Wizara hiyo itahakikisha miundombinu ya usafiri huo inakamilika kwa wakati.

“Leo (jana), tumeanza kutumia usafiri huu kwa majaribio , kila mmoja ameona umuhimu wake kwani watu wengi watafika mjini kwa wakati na kurudi Ubungo,” alisema.

Aliongeza kuwa, usafiri huo unatarajiwa kuanza rasmi Oktoba mwaka huu baada ya kutathmini bajeti nzima ya uendeshwaji wake na kujua bei ya nauli kwa wateja ambao watautumia.

Bw. Tizeba alisema bado yanahitajika marekebisho katika reli hiyo ambapo usafiri huo utakuwa ukibeba abiria 900 kwa behewa mbili ambapo treni hiyo itafanya safari mara tatu asubuhi na jioni.

Ametoa wito kwa watu waliopo maeneo ya pembezoni mwa reli kuhakikisha wanaondoka haraka iwezekavyo ili kuruhusu treni ifanye kazi ipasavyo badala ya kusubiri Serikali itumie mabavu kuwaondoa maeneo hayo wakiwemo wafanyabiashara.

Baadhi ya wananchi waliotumia usafiri huo, wamesifu juhudi za Serikali kuondoa changamoto za usafiri ambayo imeonekana kuwa kikwazo cha kufanikisha shughuli za maendeleo.

1 comment:

  1. Napenda kuipongeza serikali kwa kutimiza ahadi iliyotoa kwa wananchi kuhusu kuwepo na usafiri wa treni yya kubeba wafanyakazi kwenda na kurudi kazini katika jiji la Dar Es Salaam .

    Kwa kufanya hivi kutapunguza sana msongamano wa magari katika jiji hili linalokuwa kila siku. Aidha kwa kupunguza msongomanao huo kutapunguza matumizi ya petrol na desel kwa waendesha magari ambao walikuwa wanatumia muda mrefu kuingia na kutoka mjini.

    Pili hii itaokoa muda wa watu wanaotarajia kufanya shughuli zao kwamba wanaweza kufanya shughuli nyingine za kujenga Taifa mbali na kupoteza muda mwingi barabarani.
    Naomba juhudi hizo zielekezwe hata maeneo mengine ambayo yanaweza kujengwa reli kwa mfano kutoka jijini hadi Bagamoyo, jijini hadi Pwani /Rufiji , Kigamboni hadi Rufiji nk

    Aidha Tanzania inatakiwa itume wataalamu wake kujifunza jinsi wenzetu wa mataifa ya magharibi kama Marekani wanavyoendesha treni zao /METRO kwa ajili ya usafiri wa wafanyakazi wa mjini na Metro buses , mabasi yanayounganisha maeneo yanayozunguka reli hizo.kwa mfano katika eneo la Metropolitan yaani Washington DC, Virginia. na Maryland

    Kwa mfano liseni zinaweza kutolewa kwa wenye daladala toka maeneo Fulani ya jiji mfano Kimara hadi Ubungo kwenye vituo hivyo vya treni , mwenge hadi ubungo stesheni ili kuwapa ahueni wale wanaoshuka kwenye treni hizo za Metropolitan/ Ilala,Temeke, Dar Down town

    Treni nyingi za hapa USA zinatumia umeme basi nalo hilo mlifanyie kazi , njia mpya mtakazojenga reli zake zitumie umeme badala ya mafuta ili kwenda na wakati.
    Nampongeza waziri wa uchukuzi kwa juhudi zake hizi

    Mungu ibariki Tanzania na watu wake

    ReplyDelete