11 September 2012

JK azindua Chuo cha Ulinzi Dar



Na Salim Nyomolelo

RAIS Jakaya Kikwete, jana amefungua Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC), ambacho kitakua kikitoa mafunzo kwa maofisa wa idara mbalimbali za ulinzi na usalama pamoja na sekta binafsi.

Chuo hicho kimejengwa eneo la Kunduchi, Dar es Salaaam kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Rais Kikwete alisema chuo hicho kitasaidia mafunzo hayo kutolewa nchini badala ya maofisa kupelekwa nje ya nchi.

Alisema maofisa hao wanaweza kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kujenga mahusiano na majeshi ya nchi nyingine lakini chuo hicho kitatoa mafunzo ya ulinzi na usalama kwa ngazi za kimataifa.

“Leo ni siku kubwa kwa historia ya nchi yetu na jeshi kwa kufungua chuo hiki ambacho ilikuwa ndoto ya muda mrefu lakini tumefanikiwa,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, mwaka 1964 wasingeweza kujenga chuo hicho kwa sababu wakati huo ulikuwa ukifanyika mchakato wa kupata wanajeshi wazawa na kuliacha jeshi la kikoloni.

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Jenerali Charles Makakala, alisema chuo hicho kimeanza kutoa mafunzo kwa maofisa 20 kutoka idara tofauti za utumishi wa umma.

Alizitaja idara hizo kuwa ni pamoja na maofisa nane kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), watatu kutoka Ofisi ya Rais Tanzania Bara, wawili kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mmoja kutoka Jeshi la Magereza.

Maofisa wengine ni mmoja kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mmoja kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, mmoja kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Fedha.

Alisema mafunzo hayo yatatolewa kwa wiki 47 ambapo mafunzo hayo hutolewa katika mitaala ya aina nne na ziara ya mafunzo.

No comments:

Post a Comment