19 September 2012

Uamuzi ndoa ya Slaa kutolewa Oktoba 19


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Oktoba 19 mwaka huu inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la awali la Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, anayepinga zuio la kufunga ndoa na mchumba wake Bi. Josephine Mushumbusi, iliyofunguliwa na Bi. Rose Kamili.

Uwamuzi huo unatarajiwa kutolewa mbele ya Jaji Lawrence Kaduri anayesikiliza shauri hilo baada ya pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha hoja zao.

Katika pingamizi lake, Dkt. Slaa anayewakilishwa na wakili Bw. Philemon Mutakyemirwa, anapinga maombi ya Bi. Kamili kwa madai kuwa hakufuata taratibu za kufungua maombi yake.

Anadai kifungu namba 101 cha sheria ya ndoa, kinamtaka Bi. Kamili apeleke malalamiko yake Bodi ya Usajiri wa ndoa na si mahakamani hapo.

Aliongeza kuwa, kifungu namba 81 na 160 cha sheria hiyo, pia kinamtaka Bi. Kamili kuwasilisha maombiyake mahakamani hapo kwa hati ya kuitwa mahakamani au hati ya kiapo.

Katika kesi hiyo namba 5,2012, Bi. Kamili anapinga ndoa ya Dkt. Slaa  na Bi. Mushumbusi pamoja na kudai fidia ya sh. milioni 550 kwa gharama ya malezi ya familia na usumbufu aliopata kwa kutelekezwa na mumewe.

Dkt. Slaa na Bi. Mushumbusi walipanga kufunga ndoa Julai 21 mwaka huu, katika Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.

No comments:

Post a Comment