19 September 2012

Auawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake



Na Timothy Itembe, Tarime

MKAZI wa Kijiji cha Nyarwana, Kata ya Kibasuka, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Godfery Chegere (48), ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya watu wasiofahamika, kumpiga risasi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia juzi, miezi mitatu tangu kuuawa kwa mtoto wake Chacha Godfrey (23) na watu wanaodhaiwa kuwa majambazi.

Akisimulia tukio hilo, diwani wa kata hiyo, Selomani Moya, alisema tukio hilo linasikitisha kutokana na mazingira ya vifo vya marehemu ambao wote wameuawa kwa kupigwa risasi.

Alisema chanzo cha mauaji hayo ni familia hiyo kudaiwa kujihusisha na suala la ulinzi wa Polisi Jamii na kufanikisha kukamatwa kwa majambazi.

“Hali hii imesababisha uhasama kati ya familia hii na majambazi, naiomba Serikali ifuatilie jambo hili kwa ukaribu umakini zaidi ili wahusika wote waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola kwa kufanya mauaji ya kutisha,” alisema.

Bw. Moya alisisitiza kuwa, kama Serikali haitalivalia njuga suala hilo majambazi hao watawamaliza watu kwa kuwaua kimya kimya na zipo taarifa ya mauaji hayo kuendelea katika familia hiyo ya Mzee Kisiruti Mutwena na wengine waanaotoa siri ambazo zinachangia kukamatwa kwao.


No comments:

Post a Comment