28 September 2012
TFF kuzisaidia klabu kupata wadhamini
Na Amina Athumani
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema litazisaidia klabu zisizo na mdhamini kuandaa mpango wa biashara (Business Plan) utakaowawezesha kupata wadhamini wa kuendesha klabu zao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF , Leodger Tenga alisema ipo haja ya wadau wa soka na TFF kuzisaidia klabu zote zisizo na wadhamini kuandaa mpango huo kwa nia ya kuomba udhamini wa klabu zao.
"Kama ilivyo kwa klabu kongwe za soka hapa nchini za Simba na Yanga ambazo wao tayari wana mdhamini wao mkuu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro na klabu nyingine zinatakiwa kuwa na mdhamini, inawezekana wakawa hawajui ni vipi wafanye ili kupata mdhanini lakini asiyekuwa mshindani wa Vodacom ambao ni wadhamini wa ligi kuu,hivyo tutawasaidia kuandaa 'Business Plan' kwa wale watakaoomba msaada wa kusaidiwa,"alisema Tenga.
Kuhusiana na suala la Vodacom kuikomalia Afrika Lyon ambao wamepata udhamini kutoka kampuni ya Zantel kampuni ambayo ni mshindani wa Vodacom, Tenga alisema Lyon inaweza kumtumia mdhamini huyo katika mashindano mengine yoyote yale isipokuwa ya ligi kuu.
Alisema Vodacom imepanua wigo mpana kwa klabu kutafuta wadhamini watakaozisaidia timu isipokuwa kampuni pinzani, ambapo kuwepo kwa kipengele cha upekee kilichopo katika mkataba wa TFF na Vodacom hakiruhusu klabu kudhaminiwa na kampuni mpinzani wa vodacom katika ligi kuu.
Alisema kila kitu kipo wazi hivyo ni vyema klabu ikatafuta mdhanini asiyekuwa mshindani wa Vodacom ili kuepuka mvutano ambao kanuni zake na misingi inajieleza wazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment