11 September 2012

Tanga waunga mkono uteuzi wa Kadhi



Na Benedict Kaguo, Tanga

WAUMINI wa dini ya Kiislamu, mkoani Tanga, wameunga mkono uteuzi wa Kadhi Mkuu wa Tanzania Bara, Shekhe Abdallah Mnyasi, uliofanywa hivi karibuni na Mufti wa Tanzania , Shekhe Issa Bin Shaaban Simba.


Akizungumza na gazeti hili jana, Shekhe Mkuu mkoani hapa, Ally Juma Luwuchu, alisema uamuzi uliofanywa na Mufti Simba ulizingatia masilahi ya waumini wote wa dini hiyo nchini.

Alisema Shekhe Mnyasi ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA), ulitokana na kikao halali cha Tume ya dini kilichoshirikisha mashekhe wa mikoa na Wilaya.

“Kikao kilichompitisha Kadhi kilifanyika Juni mwaka huu, mkoani Dodoma ambaye moja ya majukumu yake ni kushughulikia masuala mbalimbali ya Waislamu,” alisema.

Aliongeza kuwa, BAKWATA tayari wameandaa mfumo wa kisheria ambao utakidhi mahitaji ya Waislamu kushughulikia kesi mbalimbali zikiwemo za mirathi na ndoa.

Alisema ni muhimu kwa mashekhe wote wa mikoa na Wilaya nchini  kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mufti Simba kuitisha kikao cha tume ya dini pamoja na kuungana ili kujiletea maendelo.

Shekhe Luwuchu alisema wakati umefika sasa WaIslam wote nchini kuitumia vizuri fursa hiyo na kuacha malumbano na badala yake washikamane kuleta maendeleo ya dini hiyo.

No comments:

Post a Comment