11 September 2012

EAC yahitaji muda kujadili maombi ya Sudani, Somalia


Na James Gashumba, EANA

NCHI wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zitaendelea kufanya mazungumzo juu maombi ya nchi mbili za Sudani Kusini na Somalia, kutaka kujiunga na jumuiya hiyo.

Nchi wanachama wa jumuiya hiyo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Uamuzi huo ulifikiwa katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri la EAC, ambalo ndio chombo cha Sera cha jumuiya hiyo, mjini Bujumbura, nchini Burundi.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya mkutano huo, vinasema baraza hilo lilikuwa na maoni kwamba, maombi ya nchi hizo ambayo yaliwasilishwa mwaka 2011 na mapema mwaka huu, yanahitaji muda zaidi ili yaweze kufanyiwa kazi.

“Baadhi ya nchi wanachama zinahitaji muda zaidi kujadiliana na wadau wote kuhusu taarifa za kamati za uhakiki juu ya maombi ya Sudani Kusini,” chazno hicho kilisema.

Ilikubaliwa kuwa, taarifa ya timu ya wahakiki iliyotumwa Juba, Julai mwaka huu, kutathmini matayarisho ya Sudani Kusini kujiunga na EAC, itawasilishwa katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri ambacho kitafanyika Nairobi, nchini Kenya, Novemba mwaka huu.

Kuhusu maombi ya Somalia, mawaziri hao walisema jambo hilo linahitaji majadiliano ya ziada na wadau zaidi wa kimataifa ambao wanajihusisha na juhudi za kuleta amani nchini humo.

Hata hivyo, Baraza lilimtaka Katibu Mkuu wa EAC kuwasilisha maombi ya Mogadishu katika kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama.


No comments:

Post a Comment